1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza njia panda: Brexit ama uchaguzi

Mohammed Khelef
4 Septemba 2019

Bunge la Uingereza linajadili muswada wa kuzuia uwezekano wa kuondoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano, huku mahakama ikikataa ombi la kumzuwia Waziri Mkuu Boris Johnson kusitisha shughuli za bunge hilo.

https://p.dw.com/p/3P0TU
Großbritannien Brexit | House of Commons, Unterhaus | Boris Johnson, Premierminister
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Taylor

Hadi sasa, kila dalili inaonesha kuwa serikali ya Waziri Mkuu Johnson inajipanga kwa ajili ya uchaguzi huo wa mapema, baada ya kura ya jana usiku kubashiri kwamba haitaweza kuruhusiwa na bunge kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya bila ya kwanza kufikia muafaka na Brussels. 

Hivi leo (Septembe 4), Waziri wa Fedha Sajid Javid amesema kuwa anafunga ukurasa wa hatua za kubana matumizi, wakati alipokuwa akielezea ongezeko la matumizi ya serikali, lakini wengi wanaamini kuwa kauli hiyo ni sehemu ya mkakati wa kushinikiza uchaguzi wa mapema wa Waziri Mkuu Johnson, ambao anaamini utaiondoa Uingereza kwenye mkwamo wa sasa kisiasa.

Kiongozi huyo wa chama cha wahafidhina, Conservatives, aliliambia bunge kwamba bado alikuwa anataka kuiondoa nchi yake kwenye Umoja wa Ulaya, ingawa angelitaka uchaguzi mpya uitishwe tarehe 15 Oktoba, siku mbili tu kabla ya mkutano wa mwisho wa kujiondoa, endapo muswada wa wabunge wanaompinga ungelishinda.

"Kwa hakika tumejitolea kutekeleza wajibu tuliopewa na wapiga kura na tutaiondoa nchi hii kutoka Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31. Ondoeni shaka kwamba tunaamuwa kwa mujibu wa sera kuipeleka nchi hii mbele na sio kuirejesha nyuma kama wanavyofanya Labour," alisema Johnson.

Muswada huo wa sheria ulitaka Johnson aombe tena miezi mitatu ya mazungumzo na viongozi mjini Brussels ili kusaka makubaliano yenye manufaa, lakini mwenyewe Johnson alishaapa kwamba kamwe asingeliruhusu hilo.

Johnson ashinda mahakamani

Karikatur | gefährdete Demokratie in UK
Katuni ya Gado ikielezea siasa za sasa za Uingereza.Picha: DW/Gado

Hayo yakijiri, mahakama mjini Edinburgh, Scotland, ilisema kwamba uamuzi wa Waziri Mkuu Johnson kulisitisha bunge usingeliweza kuzuiwa na mahakama hiyo, hukumu ambayo ilimpa nguvu mpya Johnson endapo alitaka kuitumia kuwabana wapinzani wake.

Jaji Raymond Doherty wa Mahamaka Kuu ya Session alilikataa ombi lililowasilishwa na watu watatu, akiwemo mbunge Joanna Cherry wa chama cha Wazalendo wa Scotland, SNP, ambalo liliitaka Mahakama hiyo imzuwie Johnson kulisitisha bunge. 

"Haya ni mamlaka ya kisiasa na bunge, ambayo hayawezi kupimwa kwa viwango vya kisheria, bali kwa hukumu za kisiasa. Sikubaliani na hoja kwamba kusitishwa bunge kunavunja utawala wa sheria." ulisema uamuzi wa Jaji Doherty. 

Mbunge Jolyon Maugham, ambaye pia alikuwa miongoni mwa waliotuma maombi hayo mahakamani, aliuita uamuzi huo kuwa wenye ishara mbaya.

"Ikiwa waziri mkuu anaweza kulisitisha bunge kwa siku 34, anaweza kulifanya atakavyo kwa nguvu zake za kiutendaji na mahakama haiwezi kuingilia, kwa nini asiweze kulisitisha kwa wiki 34? Kwa nini asiweze kulisitisha kwa miezi 34?" Alihoji mbunge huyo.

Uamuzi wa Johnson wa wiki iliyopita wa kupunguza siku za vikao vya bunge kabla ya muda wa mwisho wa nchi hiyo kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, Oktoba 31, ulizua hasira na ukosowaji mkubwa ndani na nje ya Uingereza.