1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haioni matumaini katika mzozo wa Ukraine

Josephat Nyiro Charo19 Novemba 2014

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alisema Jumanne (18.11.2014) haoni sababu za kuwa na matumaini kuhusu mzozo unaoendelea Ukraine kutokana na machafuko kuongezeka mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1DpaE
Steinmeier und Lawrow in Moskau 18.11.2014
Frank Walter Steinmeier (kushoto) na Sergei Lavrov mjini MoscowPicha: picture alliance/AP Photo/I. Sekretarev

Katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov hapo jana, Steinmeir alionya kuhusu hali ya kutisha inayoendelea nchini Ukraine. Alizitolea mwito pande zote zinazohusika katika mzozo wa Ukraine kuuheshimu mkataba wa makubaliano uliofikiwa katika mkutano wa mjini Minsk nchini Belarus uliofanyika Septemba 5 mwaka huu ambao kwa kiwango kikubwa unaonekana kusuasua.

Steinmeier alisema itakuwa hasara kubwa kuachana na mkataba huo ambao umefaulu kusitisha mapigano mengi, lakini umeshindwa kuepusha kuzuka machafuko ya hapa na pale katika maeneo muhimu. "Hata kama tuna shaka kama mkataba unafanya kazi katika kila kipengele, hata kama tutaripoti vipengele muhimu vimekiukwa katika wiki zilizopita, itakuwa hasara kubwa kuukataa mkataba huu. Lazima tufanye juhudi kujaribu kutafuta kilichokwenda kombo baada ya mkataba kusainiwa ili tuendeleze kazi ya kuvitekeleza vipengele hivyo."

Steinmeier alikwenda Moscow akitokea Kiev ambako alikutana na waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk. Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani alitaka kwa haraka kuwekwe eneo lisiloruhusiwa mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Ukraine na waasi wanaoegemea Urusi mashariki mwa Ukraine kuuokoa mkataba wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Russland Deutschland Gazprom Steinmeier bei Putin in Moskau
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kulia) na Waziri SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov aliunga mkono mwito wa Steinmeier na kusisitiza umuhimu wa kuutekeleza kikamilifu mkataba wa Minsk. "Lengo kuu ni kuzuia mzozo wa kijeshi kusini mashariki mwa Ukraine, kuweka eneo la kuzitenganisha pande mbili na kuondoa silaha nzito. Lakini tutatafakari njia za kuleta uthabiti wa muda mrefu Ukraine bila kusahau umoja wa taifa, maelewano na maridhiano. Na hatupaswi kuyasahau mageuzi ya katiba yaliyosainiwa na Ukraine mjini Geneva Aprili 17."

Misimamo tofauti yajitokeza

Tofauti zilijitokeza kati ya Steinmeier na Lavrov katika mkutano na waandishi wa habari huku wote wakionekana kutotulia mara kadhaa. Ingawa viongozi wote walisisitiza umuhimu wa mkataba wa Minsk, Lavrov alisema mdahalo kati ya pande zinazohasimiana Ukraine unapaswa kuzingatia uchaguzi wa Novemba 2 ulioandaliwa na waasi katika maeneo wanayoyadhibiti katika hatua ya kukaidi uchaguzi wa bunge uliofanyika siku chache kabla.

Lavrov alisema hakuna mbadala wa ushirikiano kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya akiongeza kuwa Urusi haipaswi kulaumiwa kwa mahusiano mabovu na umoja huo kwa sababu ya mzozo wa Ukraine.

Steinmeier alikutana pia na rais wa Urusi, Vladimir Putin, lakini ikulu ya Kremlin haikutoa maelezo yoyote kuhusu mazungumzo kati ya viongozi hao. Waziri Steinmeier ni kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka Ulaya kuzuru Moscow tangu mwezi Julai mwaka huu, katika ishara inayoonyesha namna gani uhusiano kati ya mataifa ya magharibi na Urusi ulivyovurugika tangu kumalizika kwa vita baridi kutokana na mzozo mashariki mwa Ukraine.

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri:Daniel Gakuba