1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haivutii wahamiaji wenye elimu ya juu

12 Julai 2010

Ionekanavyo, Ujerumani sio nchi inayowavutia sana wahamiaji, hasa wale wenye elimu ya juu. Je, Ujerumani ichukue hatua gani ili kuweza kuwavutia wahamiaji wa tabaka hiyo ya wasomi?

https://p.dw.com/p/OHWG

Kwa maoni ya wataalamu, viwango vilivyowekwa na Ujerumani ni vya juu mno,kwani nchi zingine huwavutia zaidi wahamiaji wenye elimu ya juu. Mtaalamu wa sayansi ya jamii Gunnar Heinsohn, kutoka mji wa Ujerumani, Bremen anasema kuwa Marekani, asilimia 55 ya maombi ya kutaka kuhamia nchini humo, ni kutoka watu walio na elimu ya juu: Australia ni asilimia 85,Kanada asilimia 99 na Ujerumani ni asilimia 5 tu.

Kwa hivyo wanasiasa kadhaa wa vyama ndugu vya kihafidhina serikalini, walishauri kuwekwe vigezo maalum kwa wahamiaji: Kwa mfano, wadhibiti shahada za mafunzo maalum ya kazi na wafanyiwe mitihani ya kupima akili. Fikra hizo zimezusha hasira na hata serikali ya muungano inayongozwa na vyama hivyo imetupilia mbali pendekezo hilo. Msemaji wa serikali Christoph Steegmans alieleza hivi:

"Dai kuwa wahamiaji wafanyiwe mtihani wa akili ni kosa na vile vile si fikra iliyotumia akili. Bila shaka ni ubaguzi kudhania kiholela kuwa wahamiaji ni wajinga."

Kauli hiyo inaungwa mkono pia na Barbara John, mwenyekiti wa jumuiya inayotoa huduma za kijamii. Anasema, ni sahihi kuwa Ujerumani inahitaji kuwavutia wahamiaji zaidi walio na elimu ya juu na mlango upo wazi kwa wahamiaji wa tabaka hiyo, kwani ipo sheria mpya kuhusu suala la uhamiaji. Kuambatana na sheria hiyo, anaetaka kuja Ujerumani anapaswa kuwa na kazi itakayompatia mshahara usio chini ya Euro 70,000 kwa mwaka. Au mhamiaji awe na Euro milioni moja ili apate kufungua biashara na atapaswa kuajiri hadi wafanyakazi kumi.

Kila mwaka kati ya watu 900 hadi 1,000 wanahamia Ujerumani kwa njia hiyo. Lakini kwa taifa linaloongoza duniani katika mauzo ya nje, hiyo ni hesabu ndogo mno. Kwa maoni ya Barbara John, Ujerumani inahitaji kuwavutia wahamiaji kwa maelfu.

Labda Ujerumani ingeweza kuigiza mfano wa Kanada ambapo, mhamiaji hupewa pointi kadhaa kuambatana na kiwango cha elimu, mafunzo,uwezo wa kuzungumza lugha ya nchi na kadhalika. Anaejikusanyia pointi nyingi huwa na nafasi nzuri zaidi ya kuruhusiwa kuingia nchini humo. Wataalamu wengi wangependelea kuwa na mfumo wa aina hiyo nchini Ujerumani pia.

Barbara John anasema, ule wakati ambapo Ujerumani iliweza kuchagua nani wa kuruhusiwa ndani ya nchi umepita,kwani siku hizi wahamiaji ndio wanaoamua kule wanakotaka kwenda. Na kwa hivi sasa, Ujerumani siko wanakoelekea.

Mwandishi: Riekmann,Arnd/P.Martin

Mhariri: Abdul-Rahman