1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani itatetea msimamo wake mjini Brussels

7 Februari 2013

Mkutano muhimu wa kilele kuhusu mustakbal wa Umoja wa Ulaya unalenga kuweka kando masilahi ya kitaifa,na kuafikiana kuhusu bajeti ya kugharimia miradi ya kubuni nafasi zaidi za kazi hadi ifikapo mwaka 2020

https://p.dw.com/p/17a4K
Rais wa Baraza la ulaya Van Rompuy (kulia) na Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso kabla ya mkutano wa viongozi mjini BrusselsPicha: Reuters

"Ulaya yenye nguvu bila ya kulazimika kutoa pesa zaidi":huo ndio msimamo ambao Ujerumani inatapanga kuutetea katika mazungumzo ya kubuni bajeti ya muda mrefu ya Umoja wa Ulaya.Pale viongozi wa taifa na serikali wa mataifa 27 watakapokutana kuanzia leo alkhamisi hadi kesho ijumaa mjini Brussels,serikali kuu ya Ujerumani inataka kuona gharama zote za Umoja wa Ulaya katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020 zinaambatana ipasavyo na mahitaji halisi.Matumizi bora ndio kauli mbiu ambayo kwa kansela Angela Merkel haimaanishi chengine isipokuwa kupunguzwa bajeti ya Ulaya ya mabilioni ya Euro.

Ujerumani inachangia moja kwa tano ya bajeti jumla ya Umoja wa Ulaya kiwango ambacho kinafikia Euro bilioni 200 ikizingatiwa bajeti ya kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka huu wa 2013.Wakati wa mkutano pamoja na waziri mkuu wa Italy Mario Monti hapo awali mjini Berlin,kansela Angela Merkel alikumbusha kwamba"Ujerumani ni mojawapo ya wachangiaji wakubwa miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya,Na hiyo ndio maana wanapendelea kuona kwamba fedha zinatumiwa kwa namna ambayo zitachangia ipasavyo kuufanya Umoja wa Ulaya uzidishe bidii na kuwa uwanja muhimu wa mashindano ya kibiashara."

Upinzani wa nchi za kusini mwa ulaya

Merkel und Rajoy Regierungstreffen in Berlin
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy mjini BerlinPicha: REUTERS

Hata alipokutana na waziri mkuu wa Hispania Mariano Rajoy na rais Francois Hollande wa Ufaransa,hakuchelea kansela kutilia mkazo madai ya Ujerumani,siku chache kabla ya mkutano huo wa kilele kuanza.

Sambamba na kupunguza nakisi,kanasela Angela Merkel anataka pia matumizi katika bajeti ya pamoja ya Umoja wa Ulaya yawekewe kikomo.

"Matumizi ya Umoja wa Ulaya yanabidi yasiruhusiwe kupindukia asili mia moja ya pato la kijamii katika Umoja wa Ulaya-amesema mchambuzi wa masuala ya fedha wa Umoja wa Ulaya Friedrich Heinemann wa taasisi ya uchunguzi wa kiuchumi ya mjini Mannheim.Inamaanisha kwamba bajeti ya Umoja wa Ulaya iongezeke tu ikiwa shughuli za kiuchumi za nchi za Umoja huo zitanawiri na kwa namna hiyo kuongezeka pia pato la ndani la kila mkaazi wa Umoja wa ulaya.

Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya,ikiwa ni pamoja na Austria,Finland,Itali,Uholanzi na Sweden zinauunga msimamo wa Ujerumani.Lakini nchi zinazopokea misaada mfano wa Uhispania,Ureno,Ugiriki na nyengine zinaupinga.

Ajira ya vijana ndio kipa umbele

Jugendarbeitslosigkeit
Vijana katika juhudi za kutafuta kaziPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani inataka kuona fedha nyingi zaidi zikitolewa kugharimia miundo mbinu ya nishati na miradi ya uchunguzi barani Ulaya.Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inapendekeza Euro bilioni 120 kwaajili ya miradi hiyo.Katika bajeti ya mwaka 2007 hadi mwaka huu wa 2017 asili mia 80 ya bajeti ya Umoja wa Ulaya ilikuwa ikitumika kusaidia shughuli za kilimo na miradi mengine ya kimkoa.Ujerumani ingependelea kuona fedha za kughamiria miradi ya kilimo na kimkoa zinafutwa.Katika wakati ambapo Ufaransa inataka kuona fedha hizo zinaendelea kutolewa Ujerumani inataka kuona zinatumika kupambana na ukosefu kazi miongoni mwa vijana.

Mwandishi:Fuchs Richard/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman