1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuendelea kutilia kipaumbele usalama wa Israel

Lilian Mtono
11 Oktoba 2021

Kansela wa Ujerumani anayemaliza muda wake Angela Merkel amesema suala ya usalama wa Israel litaendelea kupewa kipaumbele cha juu na kila serikali ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/41VE1
Israel Bundeskanzlerin Angela Merkel in Jerusalem
Picha: Menahem KAHANA/AFP

Kansela Merkel ametoa matamshi hayo baada ya kukutana na waziri mkuu wa Israel Naftali Bennet, katika ziara ya kuwaaga viongozi nchini Israel.

Soma Zaidi: Wajerumani kupiga kura leo kuchagua bunge na Kansela

"Kwa hivyo, kama nilivyosema, nina matumaini kwamba kila serikali ya Ujerumani, pamoja na ile inayokuja baada yangu, itajitoa kwa ajili ya usalama wa Israeli, na nadhani mrithi yeyote atakyekuwa kansela wa Ujerumani atajiona kuwa na wajibu huo." alisema Merkel.

Kansela Merkel ameongeza kuwa imani ya taifa hilo kwa Ujerumani inapaswa kujidhihirisha kila wakati.

Merkel akiwa amevalia mavazi meusi yanayoashiria maziko, pia aliweka taji la maua kwenye eneo la kumbukumbu ya mauaji ya halaiki mjini Jerusalem la Yad Vashem, na kabla ya hapo aliandika kwenye kitabu cha wageni wanaotembelea eneo hilo kwamba moyo wake huguswa kila wakati anapozuru eneo hilo.

Amesema mauaji dhidi ya Wayahudi yaliyorekodiwa mahali hapo ni ukumbusho tosha kwa Ujerumani na inavyotakiwa kuwajibika kwa Israel, lakini pia ni onyo.

Israel Bundeskanzlerin Angela Merkel zu Besuch in Jerusalem
Waziri mkuu wa Israel Naftali Bennet akiwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel walipozuru eneo la kumbukumbu ya mauaji ya halaiki la Yad Vashem Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu Bennet aliyekuwa mwenyeji wa Merkel amemuita kiongozi huyo rafiki wa kweli wa Israel. Bennet alimsifu Merkel kwa kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili na kumuelezea kama dira ya maadili ya Ulaya kutokana na hatua zake za kuiunga mkono Israel.

Alisema "Mama Kansela, tunafurahishwa sana na ziara yako hapa, ambayo ni ya saba. Unaacha uhusiano mzuri kati ya Israeli na Ujerumani, na urithi wa kutambuliwa kwa mauaji ya halaiki pamoja na kujitolea na mchango kwa usalama wa taifa la Israeli. Tunakumbuka hili, na historia itakumbuka.

Viongozi hao watofautiana kuhusu mkataba wa nyuklia wa Iran na Palestina.

Hata hivyo, pamoja na makaribisho hayo mazuri kwenye ziara hiyo ya mwisho ya siku mbili, kulishuhudiwa tofauti baina ya viongozi hao washirika katika masuala muhimu ya mkataba wa nyuklia wa Iran na kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Tofauti zao zilionekana wazi katika mkutano wao na waandishi wa habari, wakati Merkel aliposema kwamba Ujerumani itaendelea kusimamia kufufuliwa kwa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia na Iran. Hatua hiyo inapingwa vikali na Israel. Kansela aidha alisema Ujerumani bado inaamini katika suluhu la mataifa mawili kama namna bora kabisa ya kuumaliza mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

Soma Zaidi: Mpango wa Trump kuhusu Mashariki ya Kati: Dunia yatoa maoni

Bennet, anayepinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina, alitofautiana na Kansela na badala yake alisema amekuwa akiangazia hatua za kuboresha uchumi na hali ya maisha ya Wapalestina walio katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao maswahiba kutofautiana.

Hata hivyo, kwenye ziara hiyo Merkel hakupangiwa kukutana na waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani wa sasa Benjamin Netanyahu, wala viongozi wa Palestina katika eneo linalokaliwa kimabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi.

Mashirika: AFPE/APE/RTRE