1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika

22 Julai 2010

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,akisisitiza jinsi bara la Afrika lilivyo muhimu kwa Ujerumani amesema, kipaumbele kinatolewa kwa bara jirani la Afrika. Ujerumani inawajibika kisiasa, kimazingira na kimaadili.

https://p.dw.com/p/ORVc
Aussenminister Guido Westerwelle, FDP, spricht am Freitag, 9. Juli 2010, im Bundestag in Berlin. (apn Photo/Berthold Stadler) --- German foreign minister Guido Westerwelle, FDP, speaks at the German parliament Bundestag in Berlin on Friday, July 9, 2010. (apn Photo/Berthold Stadler)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guído Westerwelle.Picha: AP

Waziri Westerwelle akifanya ziara yake ya pili barani Afrika, alitamka hayo jana jioni alipowasili mji mkuu wa Uganda,Kampala. Amesema,bara la Afrika lina matatizo mengi lakini vile vile lina uwezo mkubwa. Michezo ya Kombe la Dunia imetoa sura mpya kuhusu bara zima la Afrika. Vile vile Ujerumani inatambua kuwa Afrika ni mshirika wake wa kibiashara na inataka kuimarisha ushirikiano huo pamoja na nchi za Kiafrika.Amearifu kuwa mradi maalum kuhusu bara la Afrika utaidhinishwa na serikali ya Ujerumani itakaporejea kutoka mapumziko ya majira ya joto. Waziri Westerwelle amealikwa kuhotubia mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Kampala leo hii:

"Bila shaka ni ishara ya heshima pia kwa nchi yetu kuwa nimealikiwa kama waziri wa mambo ya nje wa kwanza kuhotubia Umoja wa Afrika. Hiyo huonyesha jinsi Ujerumani inavyothaminiwa na jirani barani Afrika."

Westerwelle atakutana na mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika, Jean Ping.Vile vile kumepangwa kufanywa majadiliano pamoja na waziri mwenzake wa Uganda Sam Kutesa na Waziri wa Nje wa Malawi Etta Elizabeth Banda. Hivi sasa Malawi ndio iliyoshika wadhifa wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Mada kuu ya mkutano wa Umoja wa Afrika,ni kiwango kikubwa cha vifo vya watoto na mama wazazi barani Afrika. Hata Somalia ni miongoni mwa mada zinazoongoza katika ajenda ya mkutano huo, hasa kufuatia shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Kisomali mjini Kampala, dhidi ya washabiki wa kandanda waliokuwa wakitazama fainali ya Kombe la Dunia. Na kuhusu Somalia Westerwelle alisema:

"Ni kwelii kuwa bara la Afrika lina matatizo makubwa. Hapa ninamaanisha Somalia ambako utawala wa kisheria unazidi kupungua na matokeo yake ni vurugu tunaloshuhudia hivi sasa."

Akaongezea kuwa hali hiyo inahatarisha ulimwengu mzima kwani tatizo la uharamia linahusika na kutokuwepo kwa utawala wa kisheria nchini Somalia. Hata Sudan ni mada nyingine itakayopewa kipaumbele kwenye mkutano huo wa Umoja wa Afrika, hasa wakaazi wa Sudan wa Kusini wakitazamiwa kupiga kura ya maoni, iwapo eneo hilo ljitenge au la. Kura hiyo ya maoni imepangwa kupigwa mwezi wa Januari 2011.

Mwandishi:P.Martin/EPD

Mhariri:Josephat Charo