1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Urusi.

15 Julai 2010

Kansela Merkel asema haki za binaadamu lazima ipewe uzito nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/OJkB
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na mwenyeji wake rais Nikolas Sarkozy baada ya mkutano wao nchini Urusi.Picha: AP

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel anaendelea na ziara yake rasmi nchini Urusi na leo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Dmitry Medvedev ambaye alitoa wito kwa makampuni ya Ujerumani yasaidie kuufanya uchumi wa Urusi uwe wa kisasa ili kuwe msingi bora wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Dmitry Medvedev, baada ya mazungumzo na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, aliwaambia viongozi kutoka sekta ya biashara kwamba anatarajia sana makampuni ya Ujerumani ambayo yana uzoefu, yatashiriki katika kazi hiyo.

Akizungumza katika mji ulioko katika eneo la Urals wa Yekaterinburg, baada ya mkutano wake wa tano mwaka huu na Bibi Angela Merkel, rais Medvedev alisema akizingatia ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya kiuchumi, anaamini kuna nafasi ya uwekezaji nchini Urusi.

Ujerumani ni mshirika mkubwa wa kiuchumi wa Urusi na ina uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na taifa hilo.

Rais Medvedev pia aliwaalika wafanyabishara wa Ujerumani wawekeze katika makampuni ambayo kufikia wakati wa hivi karibuni yalikuwa hayawahusishi wawekezaji wa nje.

Mwezi uliopita Bw Medvedev alitangaza kwamba atapunguza mara tano, nambari ya makampuni yaliyotengwa na ambayo serikali ilikuwa imewekeza hisa zake hivyo kufungua njia ya kuyahusisha makampuni ya kigeni katika uchumi wa Urusi.

Rais huyo wa Urusi pia alisema serikali yake imetenga kiasi cha Dola bilioni 5.5 za Kimarekani kwa ujenzi wa kiwanda cha teknolojia katika eneo la Skolkovo, nje ya mji wa Moscow ili iwe jibu la Urusi kwa Silicon Valley, eneo la teknolojia ya juu lililoko San Francisco, California, Marekani.

Kampuni ya Ujerumani ya Siemens itatia saini baadae leo, makubaliano ya kukiendleza kituo hicho cha teknolojia cha Skolkovo.

Duru za serikali ya Ujerumani, zinasema kwamba kuna mkataba wa kima cha Euro bilioni 2.2 cha kuirugusu Ujerumani isambaze zaidi ya treni 200 kwa shirika la reli la Urusi ili kuboresha safari zake.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kwa upande wake alielezea matumaini yake ya Urusi kujiunga na shirika la biashara duniani, WTO hivi karibuni na kwamba mchango wake katika umoja wa forodha na nchi jirani kama Kazakhstan na Belarus hautazuia kujiunga kwake na shirika hilo. Urusi ambayo ilianza mazungumzo ya kujiunga na shirika hilo mwaka wa 1993, ni taifa lenye uchumi mkubwa ambalo bado halijajiunga na shirika hilo la kimataifa lenye makao makuu mjini Geneva, Uswisi.

Rais Medvedev alimhakikishia Bibi Merkel kwamba umoja huo wa forodha hautazuia mazungumzo na shirika la biashara, WTO na alitoa mfano wa mchakato wa mazungumzo ya kibiashara kati ya Urusi na Marekani.

Kansela Merkel ambaye tofauti na mtangulizi wake, Gerhard Schroeder, hakupuuza hali ya ndani ya Urusi na aligusia suala la haki za binaadam akitoa mfano wa mwanaharakati Natalya Estemirova ambaye alikutikana ameuawa katika eneo la Caucasus mwaka mmoja uliopita. Bibi Merkel alisema suala hilo ni muhimu na kwamba kazi lazima iendelee ili ujulikane ukweli.

Mwandishi, Peter Moss / AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed