1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

300810 Ukraine Janukowitsch

Josephat Nyiro Charo31 Agosti 2010

Kansela wa Ujerumani Angela amemuweka katika kitimoto rais wa Ukraine Viktor Yanukovich kuhusu suala la uhuru wa vyombo vya habari wakati alipokutana na kiongozi huyo hapo jana mjini Berlin

https://p.dw.com/p/Ozyd
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: AP

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich alileta habari njema mjini Berlin hapo jana. Bunge la nchi yake lenye idadi kubwa ya wabunge kutoka chama chake lilipitisha mageuzi ya sheria za uchaguzi kuvizuia vyama ambavyo havijamaliza mwaka mmoja tangu kuundwa visishiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu. Hatua hiyo iliwafurahisha wapinzani waliokuwa wameshinikiza kufanyika kwa mageuzi hayo.

Kwa hatua hiyo ya ushindi rais Yanukovich alisema masuala ya uhuru wa vyombo vya habari ni tete na kwamba yeye ndiye mtu anayeupa kipaumbele mchakato wa kudumisha demokrasia nchini Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema amezungumza kwa uwazi kabisa na rais Yanukovich kuhusu uhuru wa vyombo vya habari kufuatia shutuma za waandishi wa habari na mashirika ya kimataifa ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari. Amesema tangu kurudi Yanukovich madarakani maamuzi yameweza kupitishwa katika msingi imara na kuongezea,"Kwa upande mwingine nimeweka wazi kabisa kwamba kuhusiana na masuala fulani ya demokrasia, hususan uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni, tuna maswali kadhaa. Tumeyajadili masuala haya kwa uwazi kabisa."

Waandishi wa habari wa Ukraine mara kwa mara wameonya kuhusu kukanyagwa kwa haki za vyombo vya habari, wakisema shinikizo dhidi ya waandishi limeongezeka tangu rais Yanukovich alipoingia madarakani mwezi Februari mwaka huu. Hata wafanyakazi wa mashirika ya Ujerumani nchini Ukraine wamekuwa wakilalamika kuhusu idara za ujasusi nchini humo, hali ambayo inaichukiza Ujerumani kwa kuwa ina maslahi makubwa katika uhusiano na Ukraine.

Ijumaa iliyopita shirika la kimataifa la Waandishi wa habari wasio na mipaka lilimtumia barua kansela Merkel kumtaka kuvijadili vikwazo dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Ukraine wakati wa mkutano wake na rais Yanukovich. Shirika hilo lilimtaka pia ashinikize kufanyike uchunguzi wa kina kwa kupotea kwa mwandishi wa habari Vasyl Klymentev mnamo Agosti 11 mwaka huu. Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine alidokeza Alhamisi iliyopita kwamba mwandishi huyo wa jarida la kila wiki katika mji wa kaskazini wa Kharkiv, aliyekuwa akiandika ripoti kuhusu visa vya kusisimua vya rushwa, huenda aliuwawa.

Ukraine Politik
Rais wa Ukraine, Viktor YanukovichPicha: picture-alliance/ dpa/dpaweb

Kwa upande mwingine rais Viktor Yanukovich ameihimiza Ujerumani kuwekeza zaidi nchini Ukraine. Kansela wa Merkel ameahidi kuendeleza miundombinu kuiwezesha Ukraine kuandaa mashindano ya kombe la Ulaya mnamo mwaka 2012. Rais Yanukovich amemwambia kansela Merkel kwamba Ukraine inahisi inalazimika kuhakikisha usafirishaji wa gesi barani Ulaya bila kutatizwa. Bi Merkel ameahidi kuifanyia marekebisho miundombinu ya gesi ya Ukraine, kwa kuwa nchi hiyo ni muhimu katika usafirishaji wa gesi kutoka Urusi hadi barani Ulaya. Mivutano kati ya Urusi na Ukraine ilisababisha matatizo ya gesi barani Ulaya kwa wiki kadhaa mnamo mwaka jana.

Masuala mengine muhimu yaliyojadiliwa kwenye mkutano kati ya kansela Merkel na rais Yanukovich ni nia ya Ukraine kutaka kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya. Bi Merkel amesema uanachama wa NATO ni suala ambalo haliko kwenye ajenda kwa wakati huu, akisema kutatokea wakati wa kushirikiana kwa pamoja katika masuala kadhaa, mara tu jumuiya ya NATO itakapoidhinisha mkakati wake mpya utakaowezesha kuwepo ushirikiano na nchi zinazojieleza kuwa zisizo na mafungamano na upande wowote.

Kansela Merkel amesisitiza kwamba Ukraine haipaswi kuhisi inalazimishwa kuchagua kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya, akiongeza kuwa serikali ya mjini Kiev ina jukumu muhimu la kuwa mpatanishi kati ya pande hizo mbili. Akijibu rais Yanukovich amesisitiza kuwa lengo la Ukraine hatimaye kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ni ndoto muhimu kwa wananchi wake hata kama Ukraine bado ina safari ndefu.

Mwandishi: Gräßler, Bernd (DW Berlin)/ Josephat Charo

Mhariri: Thelma Mwadzaya