1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku

14 Novemba 2014

Ujerumani imezindua rasimu ya muswada ambao unaweka adhabu ya vifungo vya jela na faini kubwa kwa wanamichezo wakuu, makocha na mameneja watakaotumia au kujihusisha na dawa zilizopigwa marufuku.

https://p.dw.com/p/1Dnpy
Symbolbild Doping
Picha: picture-alliance/dpa/U. Anspach

Rasimu hiyo ya muswada bado itahitajika kujadiliwa bungeni na huenda ikapitishwa mapema mwaka ujao. Unawalenga tu wanamichezo mashuhuri, wanaofadhiliwa na fedha za serikali na walio kwenye kundi la shirika la Kitaifa la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini na hauwaathiri wanamichezo chipukizi.

Waziri wa michezo na mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere aliouzungumzia muswada huo. "Lengo la sheria hii ni kuweka kiwango kikubwa cha heshima michezoni na kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku. Tunawasilisha sheria mwafaka, sheria fupi, na sheria ya wazi lakini pia sheria kali"

Madaktari au watu wengine binafsi, watakaopatikana na virutubisho vilivyopigwa marufuku, huenda wakakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela. Katika nyakati za karibuni, wanamichezo mashuhuri wa Ujerumani wamekiri au kugundulika kutumia dawa zilizopigwa marufuku akiwemo waendesha baiskeli Jan Ullrich, Stefan Schumacher pamoja na Evi Sachebacher-Stehle, aliyegunduliwa kutumia dawa hizo katika michezo ya mwaka huu ya Olimpiki ya msimu wa baridi iliyoandaliwa mjini Sochi, Urusi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohamed Khelef