1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Marekani kuimarisha vita vyao dhidi ya ugaidi

Mohammed Khelef18 Mei 2016

Ujerumani na Marekani zinataka kuimarisha ushirikiano wao kwenye vita dhidi ya ugaidi kwa kusaini makubaliano maalum baina ya washirika hao wawili wa tangu enzi za Vita vya Pili vya Dunia.

https://p.dw.com/p/1IphR
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ujerumani, Thomas de Maiziere (kushoto), na mwenzake wa Marekani, Jeh Johnson, wakizungumza na waandishi wa habari mjini Washington.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ujerumani, Thomas de Maiziere (kushoto), na mwenzake wa Marekani, Jeh Johnson, wakizungumza na waandishi wa habari mjini Washington.Picha: Getty Images/A. Wong

Kwa mujibu wa maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili, miongoni mwa yaliyomo kwenye makubaliano hayo ni vyombo vya usalama vya nchi hizo kupeana taarifa za kiintelijensia.

"Ugaidi ni kitisho kwetu sote. Kwa hivyo tunachopaswa kufanya ni kuwa madhubuti na kusimama pamoja kimataifa," alisema waziri wa mambo ya ndani ya Ujerumani, Thomas de Maiziere, kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Washington, baada ya kukutana na mwenzake wa Marekani, Jeh Johnson.

Johnson alisema hatua ya pande hizo mbili kushirikiana dhidi ya ugaidi inaonesha imani na msimamo wa pamoja walionao dhidi ya mgogoro huo mkubwa kabisa unaoikumba dunia ya sasa.

Alikuwa akirejelea muongozo mpya wa Umoja wa Ulaya uliokubaliwa na Bunge la Ulaya mwezi Aprili, ambapo ukusanyaji wa taarifa za abiria wa ndege zitakuwa zinasambazwa kwenye nchi zote wanachama wa Umoja huo.

Baada ya mashambulizi ya kigaidi jijini Paris mwezi Novemba na yale ya Brussels mwezi Machi, Marekani ilidai kiwango kikubwa zaidi cha taarifa kutoka mataifa ya Ulaya na pia ubadilishanaji taarifa baina ya nchi zenyewe za Umoja wa Ulaya.

"Ulaya imejifunza kwa yaliyotokea mwaka jana - kutoka mashambulizi ya Paris hadi ya Brussels - na tunapiga hatua kubwa sasa," alisema de Miziere.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani alitazamiwa kukutana na Mwanasheria Mkuu wa Marekani Loretta Lynch, kujadiliana masuala ya ubadilishanaji wa taarifa za wakimbizi wanaoshukiwa kuwa na uwezekano wa kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Marekani na Ujerumani zinapanga pia kushirikiana kwenye kukabiliana na propaganga za magaidi kupitia mitandao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/DW
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman