1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani : Msukumo mpya wa kisiasa wahitajika Ukraine

17 Agosti 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steinmeier amesema Jumapili (17.08.2014) kwamba msukumo mpya wa kisiasa unahitajika kwa dharura kuyapatia ufumbuzi mapigano ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/1Cw3c
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier.Picha: Reuters

Steinmeier amesema hayo kabla ya kuanza kwa mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine mjini Berlin na kuongeza kwamba bila ya hivyo kuna hatari ya mzozo huo kuzidi kupamba moto.Steinmeir leo ana mkutano na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Urusi,Ukraine na Ufaransa mjini Berlin.

Waziri huyo amesema katika taarifa "Tunahitaji kwa dharura msukumo mpya wa kisiasa venginevyo kuna hatari ya kuingia kwenye mkwamo au kurudi tena nyuma na mzozo huo kuendelea kupamba moto zaidi."

Amesema mkutano wa Berlin utatumika kutafuta njia za kuuanzisha tena mchakato wa kisiasa jambo ambalo linamaanisha kuja na mpango juu ya namna ya kufanikisha usitishaji wa mapigano wa kudumu na udhibiti wa mipaka wenye ufanisi.

Ameongeza kusema kwamba ni kwa njia hiyo tu eneo la mashariki mwa Ukraine linaweza kuwa na utulivu na serikali ya Ukraine kuweza kuanza mazungumzo ya kitaifa ya kuwajumuisha ipasavyo kwenye jamii watu wa mashariki.

Serikali ya Ufaransa imesema inataraji mkutano huo utafunguwa njia ya kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa kilele wa amani kati ya viongozi wa Ukraine na Urusi.

Merkel ataka ukweli kutoka Urusi

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema anataka kujuwa ukweli kutoka Urusi kufuatia madai ya wapiganaji wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine kwamba wamekuwa wakipatiwa silaha na serikali ya Urusi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa msemaji wake Steffen Seibert Kansela ametowa kauli hiyo hapo jana wakati wa mazungumzo ya simu na Rais Petro Koroshenko wa Ukraine.

Madai yake yanakuja kufuatia yale yaliyotolewa na waasi wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi ambao wamekuwa kwenye uasi wa umwagaji damu mashariki ya Ukraine,kwamba wamekuwa wakipatiwa na Urusi vifaru na wapiganaji waliopatiwa mafunzo.

Seibel amesema kwamba Merkel alimwambia Poroshenko Urusi lazima iseme iwapo inawapatia waasi hao silaha au la.Hadi sasa serikali ya Urusi imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Seibert pia amesema kwamba viongozi wote wawili wa Ujerumani na mwenzake wa Ukraine wamekubaliana kwamba kupelekewa silaha kwa waasi hao hakuna budi kukomeshwa na kuwepo usitishaji wa mapigano kukomesha mzozo huo wa matumizi ya nguvu ambao umedumu kwa miezi minne sasa na kuuwa watu zaidi ya 2,100 pamoja na kusababisha janga la kibinaadamu.

Waasi wadungua ndege

Wakati mapigano yakiendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi,wapiganaji hao wanaotaka kujitenga wameidungua ndege nyengine ya kivita wakati wa usiku wa kuamkia leo. Msemaji wa jeshi la Ukraine amekiri kudunguliwa kwa ndege ya kivita chapa Mig-29 katika jimbo la Luhansk mashariki mwa Ukraine na kwamba rubani wa ndege hiyo amenusurika baada ya kuchupa.

Waasi wanaotaka kujitenga katika mji wa Luhansk mashariki ya Ukraine.
Waasi wanaotaka kujitenga katika mji wa Luhansk mashariki ya Ukraine.Picha: Getty Images/AFP/John MacDougall

Waasi hao takriban wameziangusha ndege 10 za Ukraine tokea mwezi wa Juni.

Mataifa ya magharibi pia yanawatuhumu kwa kuidunguwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia hapo Julai 17 na kuuwa watu wote 298 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Kituo cha polisi chakombolewa

Vikosi vya Ukraine leo vimepandisha bendera yao ya taifa katika kituo kimoja cha polisi katika mji wa Luhansk ambao kwa miezi kadhaa ulikuwa chini ya udhibiti wa waasi,huo unaonekana kuwa ni ushindi mkubwa katika juhudi za serikali ya Ukraine kuwatimuwa waasi hao.

Mwanajeshi wa Ukraine katika gari la deraya kwenye mji wa Donetsk mashariki ya Ukraine.
Mwanajeshi wa Ukraine katika gari la deraya kwenye mji wa Donetsk mashariki ya Ukraine.Picha: Dominique Faget/AFP/Getty Images

Maafisa wa serikali ya Ukraine wamedai kwamba waasi wamekuwa wakitapatapa kujaribu kuendelea kuushikilia mji huo wa Luhansk ambao ndio njia yao kuu ya kusafirishia mahitaji kutoka Urusi ambapo wamesema kumekuwa na ongezeko la silaha na wapiganaji wanaoingizwa Ukraine kutoka Urusi.

Urusi imekanusha kuwasaidia waasi hao na imeishutumu serikali ya Ukraine kwa kuchochea janga la kibinaadamu kwa kutumia nguvu ovyo dhidi ya watu wanaozungumza Kirusi mashariki ya Ukraine ambao wameukataa utawala wa serikali ya Ukraine.

Wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Ukraine wakikutana Berlin inaonekana kwamba mchakato huo wa kidiplomasia unaweza kutiwa kiwingu na yale yanayotokea kwa haraka katika medani ya vita mashariki ya Ukraine.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AFP/dpa

Mhariri :Yusuf Saumu