1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na China - Ushirikiano wa Kiuchumi

Zhang,Danhong/ZPR/P.Martin/RTRE10 Januari 2011

Ujerumani imefaidika sana kutokana na sekta ya viwanda iliyoimarishwa nchini China. Mataifa hayo mawili yamenufaika kutokana na mzozo wa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/QpJU
Bundeswirtschaftsminister Rainer Bruederle (FDP, l.) und der stellvertretende Premierminister der Volksrepublik China, Li Keqiang, geben sich am Donnerstag (06.01.11) in Berlin die Hand. Li Keqiang trifft waehrend seines Staatsbesuchs noch mit der Bundeskanzlerin und dem Bundespraesidenten zusammen. Foto: Michael Gottschalk/dapd
Li Keqiang, Naibu waziri mkuu wa China (kulia) na waziri wa uchumi wa Ujerumani Rainer Bruederle.Picha: dapd

Sasa pande hizo mbili zinatazamia kushirikiana zaidi huku China ikipanga kufanya mageuzi muhimu katika masoko yake ya ndani. Ukuaji wa kiuchumi nchini China unatazamiwa kupunguka kidogo lakini uchumi huo, utaendelea kuimarika.

Naibu waziri mkuu wa China, Li Keqiang anaeendelea na ziara yake barani Ulaya, amesema serikali yake mjini Beijing itatoa umuhimu kuendeleza mageuzi na kuruhusu bidhaa na huduma kutoka nchi mbali mbali duniani. Vile vile kutakuwepo uwazi na mazingira ya kuwavutia wawekezaji wa kigeni.Matamshi hayo ni kama muziki katika masikio ya mameneja wa makampuni ya Kijerumani ambayo tayari yamenufaika kutokana na uchumi ulioimarika China.

Kufuatia mzozo wa uchumi na fedha duniani,hatua zilizochukuliwa na China,zimesaidia ukuaji wa uchumi wake kwa kama asilimia 10.Baadhi ya viwanda muhimu nchini Ujerumani pia vilifaidika kutokana na ukuaji huo.

Kwa mfano,sekta ya bidhaa za elektroniki ilishuhudia ukuaji wa kama asilimia 12.Hiyo hasa ni kutokana na maagizo makubwa kutoka China.Na katika sekta ya viwanda vya kutengenezea magari, biashara ya makampuni ya VW,Daimler na BMW iliongezeka kwa takriban maradufu.Hata makampuni ya kemikali kama Bayer,BASF na Lanxess yamepata donge lake,kwani China ni mnunuzi muhimu kabisa wa bidhaa zinazotoka viwanda hivyo vya kemikali.

Vize-PM Chinas Li Keqiang zum Besuch der BMW Welt Li Keqiang und Reithofer, BMW Vorstandschef Aufnahmedatum: 08.01.2011
Li Keqiang (kushoto)alipotembelea kiwanda cha magari ya BMW, kusini mwa Ujerumani.Picha: DW

Mshauri Achim Haug wa shirika la biashara na uwekezaji la Ujerumani kwenye kanda ya Asia na Pasifik, "Germany Trade and Invest" anasema:

CLIP: HAUG:

"China ni soko kubwa kwa teknolojia ya kuhifadhi mazingira; na makampuni ya Kijerumani yanatia fora katika sekta hiyo,kote duniani. "

China inataka kuboresha miundo mbinu ya usafiri na inataka pia teknolojia ya hali ya juu. Mageuzi hayo ya kiuchumi yatahitaji vifaa bora zaidi na makapuni ya Kijerumani yataweza kutimiza mahitaji hayo.

Kwa jumla, uhusiano wa kibiashara kati ya China na Ujerumani umeimarika kufuatia mzozo wa kiuchumi na fedha.Kwa mara ya kwanza China ni muuzaji mkubwa kabisa wa bidhaa zake nchini Ujerumani na kibiashara ni mshirika wake mkubwa kabisa nje ya Umoja wa Ulaya.

Na kwa China, Ujerumani ni mwekezaji wake mkubwa kabisa kutoka bara la Ulaya.Kwa maoni ya mtaalamu Haug,nchi za magharibi vile vile hunufaika kutokana na maendeleo yanayopatikana nchini China.