1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na China zafanya mazungumzo ya kibiashara.

Sekione Kitojo29 Januari 2009

Ujerumani na China zimeanzisha mipango kuimarisha biashara, wakati kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipomkaribisha waziri mkuu wa China Wen Jiabao aliyeko katika ziara mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/GjTN
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kulia, akimsalimu siku ya Alhamis tarehe 29. Januar 2009, waziri mkuu wa China Wen Jiabao, kushoto katika ofisi ya kansela mjini Berlin.Picha: AP

Ujerumani na China zimeweka mipango leo kuimarisha biashara, wakati kansela wa Ujerumani alipomwandalia kifungua kinywa mgeni wake, waziri mkuu, Wen Jiabao, aliyeko katika ziara mjini Berlin.

Waziri mkuu Wen Jiabao alikuwa na mazungumzo hayo mjini Berlin wakati wa hatua yake ya pili ya ziara ya bara la ulaya yenye lengo la kuleta mahusiano ya kibishara na kidiplomasia katika njia sahihi baada ya hali ya wasi wasi iliyotokana na mzozo wa Tibet.



Wen Jiabao alikutana na kansela Angela Merkel , waziri wa mambo ya kigeni Frank-Walter Steinmeier, na rais Horst Koehler na alitarajiwa kufungua pia jukwaa la majadiliano kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na teknolojia.

Waziri mkuu huyo yumo katika ziara yake ya kwanza katika bara la ulaya tangu pale nchi hiyo ilipofuta mkutano uliokuwa umepangwa pamoja na Umoja wa Ulaya mwezi Desemba mwaka jana ikipinga uamuzi wa rais wa Ufaransa, Nikolas Sarkozy, kukutana na Dalai Lama , kiongozi wa kidini wa Tibet anayeishi uhamishoni.

Ziara hiyo ya siku moja nchini Ujerumani ni hatua ya pili ya ziara yake ya bara la Ulaya ambayo imemchukua hadi Uswisi ambako alihudhuria katika jukwaa la majadiliano ya kiuchumi duniani mjini Davos na pia itamchukua hadi katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels pamoja na Hispania na Uingereza.

Waungaji mkono wa Dalai Lama wamefanya maandamano mchana wa leo mbele ya ofisi ya kansela Merkel , wakimtaka kansela kutoa mbinyo kwa waziri mkuu Wen kuendelea na mazungumzo na wajumbe wa Dalai Lama.

Kansela Angela Merkel ametoa wito kama huo leo kwa waziri mkuu Wen Jiabao wakati wa mazungumzo yao, kuanzisha tena mazungumzo na wajumbe wa Dalai Lama. Ujerumani inashauku kubwa ya kurejewa mazungumzo hayo, Merkel amewaambia waandishi habari baada ya mazungumzo ya mwanzo na Wen.

Pia amesema kuwa Ujerumani iko tayari kutoa mchango muhimu katika suala hilo.

Kansela amesema pia kuwa Ujerumani haina malalamiko yoyote juu ya sera ya China moja.

Wen amesema kuna makubaliano makubwa katika mazungumzo yake na Merkel pamoja na mawaziri wake ambayo yaligusia zaidi kuhusu kuporomoka uchumi wa dunia na mzozo wa kifedha.

Wakati huo huo, China itatuma ujumbe maalum nchini Ujerumani ili kuimarisha biashara ya pande hizo mbili, amesema waziri mkuu Wen Jiabao mjini Berlin.

Wen amesema licha ya kuporomoka kwa uchumi duniani , mataifa hayo mawili yana lenga katika kuzuwia kuporomoka zaidi katika biashara baina yao, na kuongeza kuwa mwaka 2009 tunataka kuweka kiwango cha biashara kuwa kile kile kama mwaka uliopita.

Moja kati ya teknolojia ambayo China imekubali kununua katika mazungumzo ya leo ni kazi ya ubunifu ya treni yendayo kwa kasi kubwa, Transrapid, kutoka Ujerumani, mfumo wa reli ya sumaku ambayo tayari inafanya kazi mjini Shanghai ambapo China inapanga kuipanua.

Sekione Kitojo/ AFPE