1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Nigeria kuongeza ushirikiano

20 Aprili 2012

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria leo anamaliza ziara yake ya siku tatu Ujerumani. Miongoni mwa masuala aliyoyajadili na wenyeji wake ni mahusiano ya kibiashara pamoja na vita dhidi ya kundi la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/14iBe
Kansela Angela Merkel na Goodluck Jonathan
Kansela Angela Merkel na Goodluck JonathanPicha: dapd

Rais Jonathan jana alikutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Baada ya mazungumzo yao, Merkel alieleza kwamba uhusiano kati ya nchi yake na Nigeria, nchi yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika, bado una nafasi ya kukua. Rais Jonathan alisema kwamba kati ya biashara ambayo nchi yake ilifanya na nchi za Ulaya katika mwaka wa 2010, sehemu ya Ujerumani ni asilimia 2 tu. Hata hivyo, kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili mwaka jana kiliongozeka kwa zaidi ya asilimia 40.

Nigeria na Ujerumani zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati. Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Nigeria itapeleka nishati ya mafuta na gesi Ujerumani huku Ujerumani kwa upande wake ikiwekeza katika sekta ya umeme nchini Nigeria. Kansela Merkel alisema: "Ninaweza kusema kwamba katika suala la ushirika kwenye sekta ya nishati bado kuna nafasi kubwa ya maendeleo. Sisi Wajerumani sasa tuna jukumu la kuhakikisha kwamba tunafanya biashara yenye usawa."

Nigeria ina utajiri wa mafuta na gesi
Nigeria ina utajiri wa mafuta na gesiPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani yaahidi kusaidia katika kupambana na Boko Haram

Pande zote mbili zinapaswa kufaidika na mahusiano hayo ya kibiashara. Rais Jonathan hakuchoka kusisitiza kwamba kwa sasa Nigeria imetengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kutoka nje. "Zamani tulikuwa na serikali za kijeshi. Sheria ziliweza kubadilishwa wakati wowote," alisema Jonathan. "Lakini sasa mazingira ya kisiasa na ya kibiashara yameimarishwa. Wale wote waliosimamia chaguzi za kuanzia miaka ya 1998 na 1999 hadi leo wanaweza kushuhudia kwamba sasa tuko imara."

Jonathan alisisitiza pia kuwa uhalifu unaofanywa katika baadhi ya maeneo ya Nigeria na kundi la kiislamu lenye itikadi kali, Boko Haram, si hatari kwa wawekezaji kutoka nje. Mtandao mkubwa wa viongozi wa kitamaduni na wa kidini utasaidia katika kulidhibiti kundi hilo, alisema Jonathan. Rais huyo aliongeza kuwa nchi yake ingependa kuungwa mkono na Ujerumani katika vita dhidi ya Boko Haram. Kwa upande wake Kansela Merkel alisema kuwa nchi yake iko tayari kusaidia lakini akaongeza kwamba kamisheni inayosimamia uhusiano baina Ujerumani na Nigeria ndiyo itakayojadili namna ambavyo Ujerumani itaweza kuisadia Nigeria.

Shambulizi la kundi la Boko Haram katika mji wa Kano
Shambulizi la kundi la Boko Haram katika mji wa KanoPicha: Reuters

Kabla ya kurudi nchini kwake, Rais Goodluck Jonathan leo anakutana na rais Joachim Gauck wa Ujerumani.

Mwandishi: Peter Stützle

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman