1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Tunisia zatangaza makubaliano kuhusu wahamiaji

Admin.WagnerD3 Machi 2017

Ujerumani na Tunisia zimetangaza makubaliano mapya katika kukabiliana na uhamiaji unaofanyika kinyume na sheria ambapo Ujerumani itaipa Tunisia euro 250 milioni kusaidia miradi ya maendeleo katika maeneo ya kimaskini.

https://p.dw.com/p/2Yc7x
Tunesien Besuch Merkel bei Präsident Beji Caid Essebsi
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

 

Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia hali ya mvutano kati ya nchi hizo mbili kutokana na kadhia ya mhamiaji wa Tunisia aliekataliwa hifadhi nchini Ujerumani ambaye analaumiwa kwa kuendesha lori kuwaponda watu waliokuwa katika soko la Krismasi mjini Berlin ambapo watu 12 walipoteza maisha yao.

 

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amesema makubaliano hayo yatairidhisha Ujerumani na yatairidhisha Tunisia.Merkel ambaye yuko katika ziara hiyo ya siku mbili Afrika ya kaskazini akianzia Misri  hapo jana amesema Ujerumani na Tunisia zimekubaliana kuharakisha kurudishwa nyumbani kwa wahamiaji wanaokataliwa maombi ya hifadhi na suala la mafunzo ya kazi kwa Watunisia.

Amesema wamekubaliana kwamba masuala kuhusiana na utambulisho wa wahamiaji wa Tunisia wanaomba hifadhi kutoka Ujerumani yatajibiwa katika kipindi kisichozidi siku 30.Kwa mujibu wa kansela huyo pia wataisaidia Tunisia kuanzisha mfumo wa usajili ambapo itamaanisha pasipoti mpya zinazotolewa kuchukuwa nafasi ya zile za zamani zitatolewa katika kipindi kisichozidi wiki moja.  

Mpango wa kudhibiti wahamiaji     

Tunesien Besuch Merkel PK mit Beji Caid Essebsi
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza na waandishi wa habari mjini Tunis.Picha: Reuters/Z. Souissi

Ujerumani ilisema hapo awali kwamba urasimu wa Tunisia unaocholewesha mambo ndio uliopelekea kushindwa kwa nchi hiyo kumfukuza mtuhumiwa wa Tunisia Anis Amri aliyehusika na shambulio katika soko la Krismasi mjini Berlin licha ya kwamba ombi lake la kuomba hifadhi lilikuwa limekataliwa miezi sita kabla.

Akizungumza mjini Tunis Merkel ametangaza msaada wa maendeleo wa euro milioni 250 kwa nchi hiyo.

Amesema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo vijijini, biaishara za kiwango cha kati na zile ndogo ndogo nyingi  za vijana hususan wale wanaohitaji mafunzo ya kazi na fursa za ajira.Katika ziara yake hii ya nchi za Afrika Kaskazini yenye lengo la kuimarisha uhusiano na nchi hizo na kupunguza wimbi la wahamiaji wanokibimbilia Ulaya ameandamana na ujumbe wa biashara ambao yumkini ukalainisha diplomasia na uwekezaji ambao unahitakika mno na nchi kama Tunisia yenye kukabiliwa na uchumi unaozorota,mashambilizi ya wapiganaji wa jihadi na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Merkel ambaye anakabiliwa na uchaguzi hapo mwezi wa Septemba yuko katika shinikizo kupunguza idadi ya wahamiaji wanaokuja Ujerumani kutafuta hifadhi ambapo imewapokea zaidi ya wahamiaji milioni moja mwaka 2015.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman