1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Ufaransa zachukua urais wa Baraza la Usalama

Lilian Mtono
1 Aprili 2019

Ujerumani ambayo sio mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, linachukua hatamu ya urais wa baraza hilo kuanzia hii leo, ikishirikiana na Ufaransa kushikilia kiti hicho.

https://p.dw.com/p/3G0UJ
USA, New York: UN - Christoph Heusgen - Deutschland
Picha: picture-alliance/AP/R. Drew

Ujerumani na Ufaransa kwa pamoja wanahudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Ufaransa ina kiti cha kudumu kwenye baraza hilo. Ujerumani ilichaguliwa kuwa sehemu ya muhimili huo wa juu zaidi kwenye Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2019 hadi 2020. Ufaransa ilishikilia kiti hicho mwezi Machi.

Kiti hicho kinapokelewa rasmi na Ujerumani kutoka Ufaransa, lakini kiutekelezaji hakutakuwa na mabadiliko yoyote. Mashirikiano hayo yalifikiwa kati ya Berlin na Paris kama sehemu ya mkataba wa amani wa Aachen.

Kukabiliana na migogoro ni moja ya ajenda zitakazopatiwa kipaumbele. Ujerumani na Ufaransa zinataka kuendelezwa uungwaji mkono wa vikosi vinavyolinda amani nchini Mali, lakini pia kuhakikisha amani na usalama nchini Burkina Faso.

Mataifa haya yanataka pia kurahisisha mazingira ya wafanyakazi wanaotoa misaada ya kibinaadamu duniani kote kwa kuhakikisha wanajihami vya kutosha na wanalindwa. Waziri wa mambo ya nje ya Ujerumani Heiko Maas anapanga kuwasilisha mpango wa utekelezwaji wake mjini New York mwanzoni mwa mwezi huu.

Verteidigungsministerin von der Leyen in Mali
Masuala ya migogoro yatapewa kipaumbelePicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Masuala mengine yatakayotiliwa kipaumbele ni kukabiliana na biashara ya silaha ndogondogo katika eneo la Balkan na kuwawezesha wanawake wengi zaidi kushiriki kwenye siasa pamoja na kampeni za kuondoa dhuluma za kingono katika maeneo yenye mizozo.

Tangu awali, Ujerumani imeweka msisitizo wa kuliendeleza wazo la Umoja wa Mataifa la kushirikiana. Ujerumani na Ufaransa zinautumia mfumo huo wa pamoja kupinga kuongezeka kwa mitizamo mikali ya kizalendo, mfano rais Donald Trump wa Marekani. Lakini inashirikiana kuiendeleza mikataba ya kimataifa kama wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris na ule wa kukabiliana na nyuklia wa INF. 

Lakini pia Ujerumani imekuwa ikipigania kupata kiti cha kudumu kwenye baraza hilo tangu ilipoungana mwaka 1990. Ni hivi karibuni tu, kupitia mkataba wa Aachen, Ujerumani na Ufaransa walitangaza mageuzi ya Umoja wa Mataifa pamoja na kiti cha kudumu cha Ujerumani kuwa miongoni mwa malengo yao ya pamoja. Ujerumani kwa upande wake ina hoja lukuki kuhusu hilo. Miongoni mwake ni kuwa mchangiaji wa nne kwenye bajeti ya umoja huo na mfadhili mkubwa wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Mataifa.  

Haiko peke yake inayopigania mageuzi hayo. Brazil, Japan na India pia wanapambania viti vipya kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Ujerumani inatakiwa itumie vizuri nafasi hiyo, kwa sababu haitapata kiti cha kudumu wakati wowote hivi karibuni.