1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaadhimisha miaka 30 ya muungano

Grace Kabogo
3 Oktoba 2020

Ujerumani inaadhimisha miaka 30 ya kuungana tena kwa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Magharibi lakini hakuna shamra shamra kubwa kutokana na janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3jNwF
EinheitsEXPO 30. Jahrestag Deutsche Einheit
Picha: picture-alliance/dpa/A. Gora

Kansela Angela Merkel, Rais Frank-Walter Steinmeier pamoja na Spika wa Bunge, Wolfgang Schaeuble mwanasiasa mkongwe, wamehudhuria sherehe hizo rasmi zilizofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Peter na Paul kwenye mji wa kihistoria wa Potsdam, uliopo umbali wa kilometa 25 kusini magharibi ya mji mkuu, Berlin.

Wageni 130 tu ndiyo waliruhusiwa kushiriki katika tukio hilo la kanisani. Wageni walilazimika kuvaa barakoa kwenye maeneo ya Potsdam na kukaa umbali wa mita 1.5 kati yao. Takriban askari polisi 2,5000 walitawanywa ili kusimamia maandamano kadhaa yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kwenye mji huo.

Ujerumani huru na ya kidemokrasia

Akihutubia katika sherehe rasmi, Rais Steinmeier amesema Ujerumani inajivunia kuwa ''nchi huru na ya kidemokrasia'', katika miaka hii 30 tangu ilipoungana tena. Amesema hayo ni mafanikio ambayo hata janga la virusi vya corona haliwezi kuyaondoa.

''Tunatazama nyuma kwa shukrani kumalizika kwa enzi ya Vita Baridi na kuanza kwa enzi mpya. Leo tunaishi kwenye Ujerumani iliyo bora ambayo haijawahi kuwepo kabla,'' alisisitiza Steinmeier katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na Kansela Merkel, marais wa zamani wa Ujerumani Horst Köhler, Joachim Gauck na Christian Wulff pamoja na kansela wa zamani, Gerhard Schröder.

Deutschland Potsdam | Zentrale Feierlichkeiten zum Tag der Deutschen Einheit | Frank-Walter Steinmeier
Rais wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Sean Gallup/Getty Images

''Sote tulitaka kusherehekea maadhimisho ya miaka 30 ya kuungana tena kwa Ujerumani kwa njia tofauti. Pamoja na kumbi zilizojaa watu na sherehe kubwa za wazi hapa Potsdam, kukiwa na maelfu ya watu kutoka Ujerumani yote na nchi jirani za Ulaya,'' alifafanua Steinmeier.

Rais huyo wa Ujerumani amesema hata kama maadhimisho rasmi makubwa hayajafanyika, umuhimu wa siku hii unabakia pale pale na kwamba Siku ya Muungano wa Ujerumani ni wakati muhimu wa kufikiria nyuma kwa furaha na ujasiri.

Maadhimisho yalianza Septemba

Matukio kadhaa ya kuadhimisha miaka 30 ya kuungana tena kwa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Magharibi, miezi michache tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kumalizika kwa Vita Baridi, yalianza mwanzoni mwa mwezi Septemba huko Potsdam. 

Maafisa wa mji huo mwenyeji wa maadhimisho ya mwaka huu walichagua kuwa na matukio madogo, kuliko sherehe kubwa ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona. Wimbo wa taifa wa Ujerumani haukuruhusiwa kuimbwa na wageni kwenye sherehe hizo kutokana na masharti ya usafi yaliyowekwa.

Ujerumani yatimiza miaka 30 ya muungano

Katika kuelekea kwenye maadhimisho hayo, Kansela Merkel aliwashukuru wanaharakati na waandamanaji walioongoza mapinduzi ya amani ya mnamo 1989, kuuangusha Ukuta wa Berlin. ''Maadhimisho haya ni tukio kubwa la furaha na shukrani,'' alisema Merkel katika hotuba yake aliyoitoa kwenye bunge siku ya Jumatano.

Gorbachev: Mchakato ulikuwa mgumu

Kiongozi wa uliokuwa Muungano wa Kisovieti, Mikhail Gorbachev amesema sherehe hizi ni ishara kuwa migawanyiko barani Ulaya imedhibitiwa na Vita Baridi vimemalizika. Gorbachev, mshindi wa Tuzo ya Nobel, alikumbusha kwamba mchakato wa kufikia hatua hiyo ulikuwa mgumu na kwamba hatua yoyote ile ya uzembe ingeweza kusababisha mlipuko.

''Wakati Wajerumani wa Mashariki na Magharibi walipotangaza, 'Sisi ni watu,' walichohitaji kufanya viongozi wa kisiasa ni kuwa na hekima, utulivu, majadiliano na maono. Kwa Pamoja mtihani huu tuliushinda,'' alisema Gorbachev.

Hata hivyo uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni uligundua kwamba theluthi mbili ya Wajerumani hawaoni jukumu la kuungana tena kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi kama limekamilka. Wananchi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki bado hali yao ni mbaya kwa wastani ikilinganishwa na wenzao wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na shirika la Ujerumani la YouGov, kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani, GDR asilimia 83 waliona kuwa tukio la kuungana tena halijakamilika, huku kwenye maeneo yaliyokuwa Ujerumani Magharibi, walikuwa ni asilimia 59 tu.

Ujerumani Mashariki na Magharibi ziliungana tena Oktoba 3 mwaka 1990 baada ya miongo minne ya mgawanyiko uliochochewa na Vita Baridi baina ya mataifa yaliyoegemea sera za kibepari na yale yaliyozingatia siasa za ujamaa.

(DPA, AP, DW https://bit.ly/3nbjfX7)