1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaidhinisha kitita cha yuro bilioni 50 kuusadia uchumi wake

Charo Josephat13 Januari 2009

Mpango huu unalenga kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi na kulinda nafasi za ajira

https://p.dw.com/p/GXBU

Ujerumani imepitisha mpango mkubwa wa kifedha unaolenga kuzuia kuzorota kwa uchumi wake huku ulimwengu ukikabiliwa na hali ya kiuchumi. Mpango huo ulipitishwa jana na serikali ya muungano inayoongozwa na kansela Angela Merkel na kuidhinishwa na bunge la Ujerumani. Sasa unasubiri kupigiwa kura na bunge la mikoa Bundesrat.

Mpango huo wa kuupiga jeki uchumi wa Ujerumani ni wa thamani ya yuro bilioni 50 katika kipindi cha miaka miwili. Ni wa pili mkubwa katika nchi hii inayoongoza kiuchumi barani Ulaya baada ya mpango wa kwanza uliopendekezwa na kansela Angela Merkel kuusadia uchumi kuonekana kuwa mdogo mno.

Mpango huo uliokamilishwa kwenye mazungumzo yaliyomalizika jana usiku mjini Berlin kati ya chama cha Christian Democratic Union cha kansela Merkel na chama cha mrengo wa kati kinaoelemea kushoto cha Social Democratic, SPD, unajumulisha kati ya yuro bilioni 17 na 18 za uwekezaji katika miundombinu na kupunguziwa kodi kampuni na raia. Barabara na shule zitajengwa na elimu itapigwa jeki kwa kuwa ni uwekezaji wa siku za usoni.

Vipengee vingine ni pamoja na malipo kwa mtoto mmoja huku serikali ikitoa yuro 100 kwa kila mtoto. Kuna vivutio vya kuwashawishi watumiaji kununua magari mapya yaliyotengenezwa kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Mtu atayebadilisha gari yake aliyokaa nayo kwa miaka tisa kwa gari mpya atalipwa kiwango fulani cha fedha. Njia hii itasaidia kuchapusha sekta ya magari ya Ujerumani inayokabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na kulinda nafasi za ajira.

Viongozi wa makundi ya vyama vikuu katika bunge la Ujerumani Bundestag wamesema baada ya mkutano wao mjini Berlin kwamba mpango huo pia unajumulisha kupunguzwa kwa malipo ya bima ya afya ili kuwawezesha raia kuwa na fedha zaidi za matumizi.

Kiongozi wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, Volker Kauder anasema,''Kwa ujumla huu ni mpango utakaotusaidia kukabiliana na tatizo kubwa la kiuchumi, kuhifadhi nafasi za ajira na kuhakikisha kuna uthabiti nchini mwetu. Tunafahamu pia kwamba fedha hizi lazima zilipwe. Na pia kwa mujibu wa mpango huu wa kuusadia uchumi tutatafakari kuhusu vipi madeni yatakavyopunguzwa.''

Serikali ya Ujerumani pia imefungua mlango kwa kampuni kupata msaada wa kifedha kupitia mpango maalum wa kutoa mikopo na kuidhamini mikopo hiyo. Mpango wa sasa sio kama ule uliojadiliwa awali na serikali uliolenga kuzisaidia kampuni zilizoathirika zaidi kutokana na kuyumba kwa uchumi.

Lakini wanauchumi wanahofu mpango huo hautazaa matunda mengi kwa kuwa nguzo ya uchumi wa Ujerumani, yaani sekta ya uuzaji wa bidhaa katika nchi za nje inakabiliwa na matatizo makubwa huku mahitaji ya bidhaa zake katika nchi hizo yakipungua.

Takwimu za miezi ya hivi karibuni zinaonyesha kwamba uchumi wa Ujerumani unaelekea eneo la kusini la dunia huku kuagizwa kwa bidhaa za viwanda za Ujerumani katika nchi za kigeni ukiwa umepungua na uzalishaji hapa nchini ukiwa umeshuka.

Ukosefu wa ajira umeongezeka mnamo mwezi Disemba mwaka jana kwa mara ya kwanza katika miezi 33, huku idadi ya wasio na ajira ikifikia milioni tatu.

Wanauchumi wanabashiri mtu mmoja kati ya watu kumi watapoteza ajira kufikia wakati Ujerumani itakapoamua kuitisha uchaguzi mwezi Septemba mwaka huu ikiwa inataka kansela Angela Merkel aendelee kuiongoza nchi hii.

Serikali inahofu uchumi yumkini ukazorota kwa asilimia tatu mwaka huu, hivyo kuufanya mwaka 2009 kuwa mwaka mbaya zaidi tangu Ujerumani ilipojikwamua kutoka kwa uharibifu wa vita vya pili vya dunia mnamo mwaka 1949.