1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaizima ndoto ya Brazil

9 Julai 2014

Ndoto inaweza kugeuka jinamizi na la Brazil lina madhara makubwa zaidi, baada ya kupigwa kumbo kwa aibu na Ujerumani katika nusu fainali ya kombe la dunia nyumbani kwao mjini Belo Horizonte.

https://p.dw.com/p/1CYfj
Shabiki wa Brazil haamini kinachotokea katika pambano la nusu fainali Kati ya Selecao na timu ya taifa ya Ujerumani die MannschaftPicha: Reuters

Volkano haijaripuka. Wakati mabasi yakitiwa moto majiani nchini Brazil na mashabiki wakitiana ngumi,kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari, alitulia kimya.Kocha huyo mashuhuri kwa hamaki zake jana aliishiwa timu yake ilipotimuliwa kwa aibu sabaa kwa moja - timu aliyopania kuiongoza hadi kunyakua juu kabisa kombe la sita la dunia la kabumbu. Mjadala kuhusu nani atachukua nafasi yake umeshaanza.

"Nitakumbukwa kama kocha aliyepigwa kumbo 7-1." Jukumu lake la kuwatunukia Wabrazil milioni 200 taji la ubingwa wa dunia nyumbani limeshindwa. Badala yake amewaomba radhi wananchi kwa makosa yaliyotokea. "Miye ndiye dhamana kwa yale yaliyowasibu Selecao uwanjani," amesema kocha huyo.

Hatima ya Scolari haijulikani

"Magoli 7-1 si matokeo ya kawaida kati ya wababe wa dimba ulimwenguni," ameungama kocha wa timu ya taifa ya Argentina, Alejandro Sabella, ambaye timu yake inateremka leo usiku katika pambano la pili la nusu fainali dhidi ya Uholanzi mjini Sao Paulo .Atakayeibuka na ushindi katika pambano hilo ndie atakaepimana nguvu na Ujerumani Jumapili ijayo.

FIFA WM 2014 Deutschland vs Brasilien 08.07.2014
Kocha wa timu ya taifa ya Brazil Scolari akimtuliza Oscar (kushoto) asiliePicha: Reuters

Jumamosi itakuwa zamu ya kuwania nafasi ya tatu na Scolari bila ya shaka ataketi uwanjani. Baadaye itakuwa mwisho wa hadithi ya mtoto huyo wa mkulima wa Kitaliana aliyeiongoza Brazil mwaka 2002 hadi kunyakuwa Kombe la Dunia.

Ilikuwa miaka 12 iliyopita, upepo unavuma upande mwengine na walioashiria kuwa wanasoka wa Amerika Kusini ni muhali kushindwa nyumbani wamekosea.

Löw akumbusha kiunzi cha mwisho Jumapili

Magoli 7-1 kwa Ujerumani ni matokeo yanayomtoa nyoka pangoni. Mwenyekiti wa Shirikisho la Kabumbu la Ujerumani, Wolfgang Niersbach, anasema: "Ni siku ya kihistoria kwa kabumbu la Ujerumani na ulimwengu kwa jumla. Ustadi ulioje - maneno pekee hayatoshi kulisimulia. Ukisema la kusisimua pia haitoshi. Jukwaani watu wakikodolea macho. Ni kabumbu kutoka sayari nyengine. Lakini bora tusitie chumvi, Jumapili inatusubiri ili kuweza kukiuka kiunzi cha mwisho."

WM 2014 Halbfinale Deutschland Brasilien Hamburg Public Viewing
Mashabiki wa timu ya taifa ya Ujerumani wakifuatilizia pambano la nusu fainali katika uwanja wa Heiligengeist mjini HamburgPicha: picture-alliance/dpa

Kauli kama hiyo imetolewa pia na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Löw, ambaye mbali na kusifu ujasiri, ustadi na shauku amekumbusha Jumapili ijayo wanabidi wajizatiti zaidi ili kukamilisha ndoto ya mashabiki na wapenzi wa soka ulimwenguni.

Wadadisi wa soka wanakubaliana kama kuna watakaoweza kuondoka na kombe la dunia uwanjani,mamoja mshindi atakuwa nani kati ya Uholanzi na Argentina,basi wajerumani.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/SID/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman