1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakabidhi kambi ya Kunduz,Afghanistan

6 Oktoba 2013

Baada ya kipindi cha miaka kumi jeshi la Ujerumani Bundeswehr Jumapili(06.10.2013) limekamilisha jukumu lake kaskazini mwa Afghanistan kwa kukabidhi rasmi mamlaka ya kambi yao ya Kunduz kwa vikosi vya Afghanistan.

https://p.dw.com/p/19uT3
Mawaziri wa Ujerumani na Afghanistan wakishuhudia wakati maafisa waandamizi wa kijeshi wa Ujerumani na Afghanistan wakisaini nyaraka za makabidhiano ya kambi ya Kunduz.
Mawaziri wa Ujerumani na Afghanistan wakishuhudia wakati maafisa waandamizi wa kijeshi wa Ujerumani na Afghanistan wakisaini nyaraka za makabidhiano ya kambi ya Kunduz.Picha: Reuters

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kwa pamoja wameikabidhi kambi hiyo kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan katika ziara isiotangazwa iliofanyika Jumapili wakitokea kwenye kambi ya jeshi la Ujerumani ya Mazar-i-Sharif. Akizungumza katika hafla hiyo de Maiziere amezungumzia juu ya kujitolea roho zao kwa wanajeshi wa Ujerumani huko Kunduz ambapo 18 wameuwawa kutokana na mashambulizi na katika mapambano wakati wa kutimiza majukumu ya Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi (ISAF) chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.Amesema "Kwetu sisi Kunduz ni mahala ambapo Bundeswehr ilipigana kwa mara ya kwanza na ilibidi kujifunza kupigana.Huo ulikuwa wakati muhimu wa maamuzi sio tu kwa jeshi la Ujerumani bali pia kwa jamii ya Ujerumani."

Waziri huyo amesema juu ya kwamba jeshi la Ujerumani linaondoka katika jimbo hilo amesisitiza kwamba katu hawatolisahao kwa kuwa lina umuhimu mkubwa wa kiishara kwa jeshi la Ujerumani. Amesema Kunduz ni mahala ambapo imelishughulisha jeshi la Ujerumani kuliko mahala popote pale,hapo walijenga na kupigana,walilia na kujifariji,waliuwa na kuuliwa. de Maiziere amesema "Kunduz daima itakuwa sehemu ya kumbukumbu yetu ya pamoja."

Jukumu la usalama ni zito

Idadi ya wanajeshi 18 wa Ujerumani waliouwawa huko Kunduz kutokana na mashambulizi na wakati wa mapigano ni kubwa kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (kutoka kushoto kwenda kulia ),Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afghanistan Mohammad Omar Daudzai, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afghanistan Enayatullah Nazari wakibadilishana funguo za ishara wakati wa makabidhiano ya kambi ya Kunduz.(06.10.2013)
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (kutoka kushoto kwenda kulia ),Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afghanistan Mohammad Omar Daudzai, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afghanistan Enayatullah Nazari wakibadilishana funguo za ishara wakati wa makabidhiano ya kambi ya Kunduz.(06.10.2013)Picha: Reuters

Kwa jumla wanajeshi 54 wa Ujerumani wameuwawa nchini Afghanistan 35 kati yao wamepoteza maisha yao kutokana na mashambulizi na mapambano wengine wamekufa kutokana na ajali au kujiuwa. De Maiziere amelitaka jeshi na polisi wa Afghanistan wachukuwe jukumu la usalama katika jimbo hilo lenye vurugu ambao hivi sasa ni wajibu ulioko moja kwa moja mikononi mwao. Amesema wanataraji na kutegemea kwamba vikosi vya usalama vya Afghanistan vitadumisha usalama huko Kunduz na ikibidi kurudisha usalama kwenye maeneo yalio karibu na jimbo hilo. Ameongeza kusema "Majukumu tunayowakabidhi nyinyi washirika wetu wa Afghanistan ni mazito. Ujerumani inafahamu inamaanisha nini na naheshimu sana ushujaa na ujasiri wa wanajeshi na polisi wa Afghanistan."

Katika kambi hiyo kutawekwa kikosi kimoja cha wanajeshi wa Afghanistan pamoja na polisi wa kuzuwiya fujo.Hali ya usalama katika jimbo hilo lenye vurugu hivi karibuni imezidi kuwa mbaya, wanasiasa kadhaa mashuhuri wameuwawa na kundi la wanamgambo wa itikadi kali wa Kiislamu la Taliban katika wiki za hivi karibuni.Pia mashambulizi ya vituo vidogo vya wanajeshi wa usalama wa eneo hilo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara.Waafghanistan wengi wanahofu kwamba hali itazidi kuwa mbaya wanajeshi wa Ujerumani watakapondoka kutoka Kunduz.

Ujerumani haitoiacha mkono Afghanistan

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametumia hotuba yake katika hafla hiyo ya Jumapili kuahidi kuendelea kwa Ujerumani kuisaidia Afghanistan baada ya kuondolewa kwa vikosi vyake vya kivita.Amesema" Kazi yetu ya kujenga mustakbali mwema kwa Afghanistan haimaliziki hapa.Tutaendelea kuisaidia Afghanistan katika shughuli za kiraia."

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere (wa pili kushoto) na Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (wa pili kulia) wakiwasili katika kambi ya Kunduz.(06.10.2013).
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere (wa pili kushoto) na Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (wa pili kulia) wakiwasili katika kambi ya Kunduz.(06.10.2013).Picha: Reuters

Ujerumani imeahidi kutowa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2016 euro milioni 430 kwa mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini Afghanistan. Ziara ya Jumapili ni ziara ya kwanza kufanywa kwa pamoja na waziri wa ulinzi wa Ujerumani de Maiziere na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Westerwelle katika nchi hiyo ilioathiriwa na vita juu ya kwamba wote wawili waliwahi kufanya ziara kadhaa nchini humo katika nyakati tafauti wakiwa kwenye nyadhifa zao hizo za sasa. Kwa Westerwelle inaonekana hiyo itakuwa ziara yake ya mwisho kwa kuwa chama chake cha kiliberali cha Freedom Demoktatik (FDP) kimeshindwa kukiuka kiunzi cha kujipatia asilimia tano ya kura katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliofanyika tarehe 22 mwezi wa Septemba ili kuweza kuwakilishwa bungeni. Pia haifahamiki de Maiziere atakuwa na dhima gani katika serikali mpya ya mseto chini ya uongozi wa Kansela Angela Merkel.

Wanajeshi wa Ujerumani walioko Afghanistan

Kwa jumla hivi sasa Ujerumani ina takriban wanajeshi 4,000 kaskazini mwa Afghanistan kama sehemu ya kikosi cha ISAF.Kuna wakati wanajeshi wa Ujerumani waliowekwa nchini Afghanistan walifikia 5,300.Vikosi vyote vya mapambano vya ISAF vitaondolewa nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014 wakati vikosi vya Afghanistan vinapotazamiwa kuchukuwa majukumu ya usalama kwa nchi nzima.

Jeshi la Ujerumani likiwa kwenye doria mashariki ya Kunduz.
Jeshi la Ujerumani likiwa kwenye doria mashariki ya Kunduz.Picha: AP

Ujerumani imeahidi kutowa hadi wanajeshi 800 kwa Afghanistan baada ya mwaka 2014 wakati kikosi cha kimataifa cha kutowa mafunzo kitakapochukuwa nafasi ya Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama (ISAF). Wanajeshi wote 900 wa Ujerumani waliobakia huko Kunduz wanatakiwa wawe wameondolewa kwenye kambi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu. Juu ya kwamba sehemu ndogo ya kambi hiyo itabakishwa kwa ajili ya takriban wanajeshi 300 wa Ujerumani pindipo wakihitajika kuwekwa kwa haraka.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa/AFP/DW

Mhariri: Bruce Amani