1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakumbuka fadhila

18 Januari 2013

Ubalozi wa Ujerumani mjini Kigali umeikabidhi serikali ya Rwanda mabaki ya kihistoria katika vita vya kwanza vya dunia mwaka 1914. Mabaki hayo ni magurudumu mawili ya magari ya kivita ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/17My6
Mitaa ya mji mkuu wa Rwanda Kigali
Mitaa ya mji mkuu wa Rwanda KigaliPicha: flickr/noodlepie

Kuna pia picha za wanajeshi wa Rwanda waliosaidiana na wanajeshi wa kijerumani na mikanda ya filamu na picha zinazoonyesha wanajeshi wa Rwanda na Wajerumani waliopambana katika vita hivyo. Balozi wa Ujerumani nchini Rwanda, Peter Fahrenholtz, amesema wanategemea pia kufukua mabaki ya meli ya kijerumani iliyozamishwa na wanajeshi wa Kijerumani kwenye ziwa Kivu linalotenganisha nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Historia

Balozi Peter Fahrenholtz ndiye aliyekabidhi mabaki ya gari hilo la kivita kwa mkuu wa mamlaka za maktaba za taifa kwa ajili ya masalio ya kihistoria.

Maktaba hiyo ya kihistoria maarufu kwa jina la Richard Kandt iko mjini Kigali na ilipewa jina hilo kwa hisani ya Mjerumani Richard Kandt ambaye inaaminika ndiye aliyejenga nyumba ya kwanza mjini Kigali mwaka 1907 mwaka ambao mpaka leo inaaminika ndipo ulipoanza kujengwa mji huu mkuu wa Rwanda.

Mabaki hayo ni pamoja na magurudumu mawili ya gari la kivita lililotumiwa na wanajeshi wa Ujerumani yenye uzito wa kilo 500.

Mabaki mengine ni pamoja na picha na filamu za wanajeshi wa Rwanda wa wakati huo walioshirikiana na wajerumani kupigana vita na wabelgiji waliokuwa wametoka Congo wakati huu ikiwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Deutsche Wehrmacht in Jugoslawien
Picha: AP

Mabaki hayo yalivumbuliwa na Mjerumani mwingine Dr Reinhart Bindseil eneo la Gisenyi karibu na mpaka wa DRC na Rwanda kwenye mwaka ambao hata hivyo haukutajwa.

Ushirikiano Ujerumani na Rwanda

Balozi wa Ujerumani nchini Rwanda Peter Fahrenholtz amesema hii ni ishara ya ushirikiano wa muda mrefu baina ya Rwanda na Ujerumani.Balozi huyo amesema kwamba kwa sasa anataka kuwahamasisha wawekezaji wa kijerumani kuja kwa wingi kuwekeza nchini Rwanda.

''Kitu ambacho tunaweza kukifanya Rwanda na Ujerumani kwa pamoja ili kuimarisha mafungamano yetu ni kuhakikisha ninawaleta wawekezaji wakubwa wa kijerumani kuwekeza hapa na bila shaka hii itaongeza nafasi za ajira''

Mkuu wa mamlaka za taifa kuhusu historia Alphonce Umulisa amesema kwamba mafungamano ya Rwanda na Ujerumani ni ya kihistoria na kuwahimiza wananchi kulitembelea jengo hilo ili kujua zaidi juu ya historia ya nchi mbili Rwanda na Ujerumani.

Gedenktag zu Ehren der Kriegsveteranen
Makumbusho ya waliopigana vita vya pili vya dunia Sai WanPicha: Reuters

''Hii ni ishara na ushahidi wa historia ya jinsi wanyarwanda walivyoweza kupambana juu ya kuitetea nchi yao.Huu ni wakati muafaka wa kila mwananchi kuja kujionea jinsi mababu zetu walivyopambana, picha hizi zinaonyesha waziwazi na imesekana jinsi walivyoshirikiana na wajerumani huu ni ushahidi tosha''

Vilevile balozi wa Ujerumani amesema siku zijazo watapeleka mabaki ya meli nyingine ya kivita iliyozamishwa makusudi na wanajeshi wa Ujerumani kwenye ziwa Kivu wakati wa vita hivyo na wabelgiji ilikuwa mwaka 1916.

Lakini mabaki ya meli hiyo bado yako kwenye ziwa Kivu na hakubainisha ni lini shughuli za kuiopoa meli hiyo zitaanza wakati gani.

Ujerumani imekuwa ikitoa misaada kwa Rwanda kwenye miradi ya miundombinu mathalan kwenye shughuli za uzalishaji nishati.

Mwandishi: Sylivanus Karemera

Mhariri: Josephat Charo