1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaomboleza watu 80,000 waliokufa kwa Corona

Bruce Amani
18 Aprili 2021

Ujerumani Jumapili imeandaa siku ya kitaifa ya kumbukumbu kwa ajili ya wahanga karibu 80,000 wa janga la virusi vya corona nchini humo.

https://p.dw.com/p/3sC4C
Berlin Konzerthaus am Gendarmenmarkt | Rede Steinmeier | Gedenkfeier Covid-Opfer
Picha: Michael Sohn/AFP/Getty Images

Rais Frank-Walter Steinmeier na Kansela Angela Merkel wamehudhuria hafla za kumbukumbu wakati nchi hiyo ikishuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona

Viongozi hao wawili kwanza walishiriki katika ibada ya asubuhi katika Kanisa la Kumbukumbu la Kaiser Wilhelm mjini Berlin.

Soma pia: Idadi ya vifo vya COVID-19 duniani yapindukia milioni 3

Nini alichosema rais?

Steinmeier alitoa wito kwa umma kuwakumbuka waliouawa, akiwaomba "kuzingatia maafa ya kibinaadamu katika janga hilo.”

Coronavirus | Berlin Kaiser-Wilhelm-Gedächtnis-Kirche | Gedenken für Covid-Opfer
Ibada ya kumbukumbu ilifanywa BerlinPicha: Gordon Welters/Pool KNA/AP/picture alliance

Rais huyo amesema "inaeleweka” kuwa "tumekuwa tukihangaika kuhusu viwango vya maambukizi na idadi ya vifo kila siku.”

Lakini ana hisia "Kuwa sisi, kama jamii, hatujajikumbuka vya kutosha kila wakati kuwa hatima za kibinafsi, maisha ya binaadamu, yapo nyuma ya takwimu hizi zote.”

Ameonya kuwa "jamii inayopuuza mateso itateseka kwa ujumla.”

Kuwakumbuka waliokufa wakiwa peke yao

Steinmeier pia aliwataja wale waliofariki wakiwa peke yao au waliokosa nafasi ya kusema kwaheri ya mwisho wakiwa hospitalini kutokana na vizuizi vya janga hilo vilivyowekwa.

Soma pia: Ujerumani kuweka sheria ya kitaifa kudhibiti COVID-19

"Kufariki katika wakati wa janga aghalabu huwa ni kifo bila kwaheri inayostahiki. Wakati mwingine hata wanafamilia hawakuruhusiwa kuwatembelea wapendwa wao hospitalini au makaazi ya malezi. Watu wengi wamekufa bila hata jamaa zao na marafiki kuweza kuwaambia kwaheri.”

"Wengine walipata uchungu mwingi sana kwa sababu walinyimwa fursa ya kuwaona au kuwagusa kwa mara ya mwisho waliofariki.”

Amesisitiza kuwa siku ya kuomboleza itawakumbusha watu kuwa "hawako peke yao katika majonzi, hawako peke yao katika kuomboleza.”

Idadi ya vifo yatarajiwa kuongezeka katika wimbi la tatu Ujerumani

Hafla ya Jumapili imekuja wakati maafisa wa afya wakionya kuwa wengi watafariki kutokana na virusi hivyo.

Soma pia Ujerumani yakubaliana hatua sawa kudhibiti corona

Lothar Wieler, rais wa Taasisi ya Ujerumani ya Afya ya Umma ya Robert Koch amesema hali katika vyumba vya wagonjwa mahututi inaendelea kuwa mbaya, na katika matukio mengi, sasa wanawatibu wagonjwa katika kundi la watu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49

AFP