1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatolewa dimba la Ulaya kwa wanawake

Bruce Amani
31 Julai 2017

Matumaini ya Ujerumani kutwaa taji la saba la mfululizo katika dimba la Ulaya kwa wanawake yalisambaratishwa jana baada ya Denmark kuwafunga mabao mawili kwa moja katika robo fainali mjini Rotterdam.

https://p.dw.com/p/2hS3h
Niederlande Frauen-Fußball-EM in Rotterdam - Deutschland vs. Dänemark
Picha: Getty Images/M. Hitij

Denmark ilifunga mabao yake mawili kwa njia ya kichwa katika kipindi cha pili kupitia wachezaji Nadia Nadim na Theresa Nielsen. Sara Däbritz ni mchezaji wa timu ya Ujerumani na anasema wanapaswa kujilaumu kwa matokeo hayo "tulianza mechzo vizuri sana na tukawa kifua mbele kwa bao moja, ambalo lingetupa nguvu kiasi za kuendelea, lakini taratibu tukaufanya mchezo kuwa rahisi kwa Denmark.

Ujerumani, ambao wameshinda dimba la Euro mara sita mfululizo, na mataji manane kwa ujumla, walitawala mchezo huo ulioahirishwa kutoka Jumamosi kwa sababu ya mvua kubwa, lakini mchezo wa mashambulizi ya kushtukiza wa Denmark ndio uliwaangamiza. Ujerumani haikuonekana kuwa imara katika mechi zake za dimba hilo na Kocha Steffi Jones amesema ni wakati wa kuutathmini mfumo walioutumia "Bila shaka sasa nnayakosoa maamuzi yangu. Kwanza nachunguza kila kitu kilivyokuwa, na kisha tunaweza kuona kama mfumo huu ulifaa, au kama tungeuchagua mwingine."

Michuano ya nusu fainali itachezwa Alhamisi, ambapo Denmark itashuka dimbani dhidi ya wageni Austria ambao waliwanyamazisha Uhispania kwa kuwafunga penalti 5-3 baada ya mechi kutoka sare ya bila kufungana mjini Tilburg.

Wenyeji wa dimba hilo Uholanzi, ambao waliwafunga Sweden 2-0 siku ya Jumamosi, watacheza na England ambao waliwafunga Ufaransa 1-0 mjini Deventer hapo jana. Ulikuwa ushindi wa kwanza wa England dhidi ya Ufaransa katika miaka 43.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri:Yusuf Saumu