1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu dhidi ya ubinadamu, Guinea

Abdu Said Mtullya22 Desemba 2009

Umoja wa Mataifa wasema viongozi wa utawala wa kijeshi nchini Guinea wanapaswa kuwajibika kisheria kwa sababu ya kutenda uhalifu.

https://p.dw.com/p/LAu5
Askari wa utawala wa kijeshi nchini Guinea.Picha: AP

Umoja wa Mataifa umesema viongozi wa utawala wa kijeshi wa Guinea wanapaswa kujibu tuhuma juu kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu.Umoja wa Mataifa umesema hayo baada ya uchunguzi uliofanywa na tume yake kuthibitisha utambulisho wa watu 156 waliouawa na waliopotea nchini Guinea.

Umoja huo umesema kuuawa kwa wapinzani wa serikali mnamo mwezi wa septemba ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kwamba viongozi wa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo wanapaswa kuwajibika kisheria.

Tume ya Umoja huo iliyofanya uchunguzi nchini Guinea imethibitisha utambulisho wa watu waliouwa na waliopotea kufuatia mashambulio yaliyofanywa na askari watiifu kwa kiongozi wa utawala wa kijeshi kapteni Moussa Dadis Camara. Watu hao walishambuliwa kwenye uwanja wa michezo,mjini Conakry walipokuwa wanashiriki kwenye mkutano wa hadhara wa kupinga mpango wa kapteni Camara wa kukusudia kuwania kushiriki katika uchaguzi wa rais.

Uchunguzi wa tume hiyo pia umeonyesha kwamba wanawake 109 walibakwa na walifanyiwa matendo mengine ya ukatili ikiwa pamoja na kukeketwa na kudhalilishwa kitumwa.

Ripoti ya tume ya Umoja Mataifa imesema uhalifu huo ulitendwa na askari wa utawala wa kijeshi wakati walipowashambulia wananchi walipokuwa wanaandamana.Tume hiyo imedai kwamba akina mama na wasichana walipelekwa kwenye makao ya jeshi na kwenye nyumba za maafisa wa kijeshi ambako waligeuzwa watumwa wa ngono kwa siku kadhaa.

Katika ripoti yake tume ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban- Ki-moon imesema inawezekana kutamka kwa uhakika kwamba uhalifu uliotendwa tarehe 28 mwezi septemba na katika siku zilizofuatia, ulikuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Umoja wa Mataifa umesema pana sababu za kuamini kwamba kapteni Kamara, mpambe wake pamoja na waziri wake, anaeshughulikia majukumu maalum wanapaswa kuwajibika mbele ya sheria kwenye vyombo vya kimataifa.

Tume imependekeza , Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litilie maanani hali ya nchini Guinea.

Mwandishi/Mtullya/AFPE/ZA

Mhariri/Othman, Miraji