1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukosefu wa Mipango Miji kuleta Madhara zaidi

8 Agosti 2010

Utafiti mpya wa Taasisi ya Mazingira na Maendeleo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) umeonya kuwa mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea wataathirika na ukosefu wa mipango miji.

https://p.dw.com/p/OeyE
Alltag in Kibera, dem größten Slum von Afrika. Das Bild entstand während einer Koproduktion von KBC und DW im November 2006 in Nairobi. Uebertragung der Rechte dieses Bildes an DW-Online Aufnahme von Maja Dreyer (DW). Die Verwendung des Bildes ist für die Verwendung im gesamten Online-Angebot der Deutschen Welle gestattet.
Kibera, nchini Kenya, kitongoji duni cha pili kwa ukubwa barani Afrika.Picha: DW

Madhara hayo ya umaskini uliosababishwa na upangaji mbaya wa miji na magonjwa yanayohusiana na mazingira, kama vile kipindupindu, yatatokea iwapo viongozi wao hawatochukuwa hatua na kupanga mipango na mapema ya kukabiliana na kukua kwa haraka kwa makaazi ya miji.

Maelfu ya Wakenya wanaoishi mijini matajiri na maskini wanaishi katika hofu kwamba nyumba zao au uwekezaji wao wa majengo unaweza kubomolewa hivi karibuni wakati nchi hiyo ikihangaika kukabiliana na kuongezeka kwa haraka kwa makaazi ya miji.

Wakenya wengi matajiri na maskini tayari wameathirika na hali hiyo. Katika eneo la makaazi ya kifahari la Nairobi la Spring Valley, Mike Maina Kamau aliamka tarehe 14 ya mwezi wa Julai kukabiliana na ukweli wa idhara, ambapo maafisa wa serikali walikuwa wakiibomowa kwa matinga tinga nyumba yake ya kifahari ya vyumba vinane iliokuwa na thamani ya dola milioni 13.

Hata hivyo, yeye sio mtu pekee yaliyomsibu hayo.Matukio kama hayo yamekuwa yakiendelea kutokea kwa miaka mingi.Majengo mengi yamebomolewa ikiwa ni pamoja na vituo vya mafuta,maduka,nyumba za kuishi watu,vioski vidogo na nyumba zisizo rasmi.Hatua hiyo imechukuliwa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutanua mji. Mojawapo ya kumbukumbu kubwa kabisa ya bomoa bomoa hiyo ilikuwa mwezi wa Oktoba mwaka 2008 wakati mojawapo ya supamaketi kubwa kabisa nchini humo ,kandoni mwa barabara ya Thika ilipobomolewa wakati wa usiku.Mali yote ya thamani ya mamilioni ya dola iliokuwemo ndani ya duka hilo la Nakumatt iliangamia.

Haja ya kutanuwa barabara katika mji wa Nairobi, hususan karibu na mji huo kutokana na mson´gamano mkubwa wa magari wakati wa saa za harakati ,ndio kiini cha tatizo hilo ambapo ilibidi wapangaji miji wende kupekua ramani za kale kutafuta mipango ya barabara ya zamani kwa ajili ya kuzitanua.

Ndipo wajenzi na wamiliki wengi wa majengo walipokuja kutanabahi, kwamba licha ya kupata mali hizo kwa kupitia kile kilichoonekana kama taratibu za kisheria kutoka serikali iliopita, nyingi ya hati hizo zilitolewa na maafisa wa serikali wala rushwa na kwamba hawana haki ya kisheria kwa ardhi wanazomiliki na majengo yao yakavunjwa kutowa nafasi ya kutanuliwa kwa barabara.

Utafiti mpya unaonya kwamba iwapo serikali katika nchi zinazoendelea hazitochukua hatua na kuwa na mipango miji zitahatarisha mustakbali wa mamia kwa mamilioni ya wananchi wake hususan Afrika na Asia.

Serikali hizo zimetakiwa kujifunza na kile kinachotokea Brazil kwa kutokuwa na mipango miji ambako kutokana na kuongezeka kwa haraka kwa makaazi ya miji nchini Brazil, umaskini umezidi kukithiri na matatizo mapya ya kimazingira yameibuka.

G51502 Kenia, Nairobi Kenia Nairobi Kenyatta, Jomo Denkmal und Konferenzzentrum Architektur Afrika Kenya city square monument congress center
Kituo cha mikutano cha Jomo Kenyatta mjini Nairobi,Kenya.Picha: picture-alliance / Helga Lade Fo

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa jaa la taka la Dandora lilioko Nairobi ni mojawapo ya jaa kubwa kabisa barani Afrika. Jaa hilo lilianzishwa miaka ya 1970 kama hatua ya muda lakini wakati jiji limendelea kutanuka jaa hilo limebaki kama lilivyo na taka zote za Nairobi zinatupwa hapo zikiwemo zile za kemikali.Jaa la Dandora linahusishwa na kuwepo kwa afya mbaya hususan miongoni mwa watoto wa hapo na ni mchafuzi mkuu wa Mto Nairobi.

Inaelezwa pia kwamba vibanda vilioko kwenye kitongoji duni cha Kibera mjini Nairobi vimekaliana sana kwamba hakuna hata nafasi ya vyoo na wakaazi inabidi wende haja kwa kutumia mifuko ya karatasi na baadae kuitupilia mbali,hali hiyo na ukweli kwamba hakuna mfumo wa maji taka katika kitongoji hicho, jambo hilo linakuwa chanzo cha mripuko wa magonjwa.

Kibera ni kitongoji duni cha pili kwa ukubwa barani Afrika, kikitanguliwa na Soweto, Afrika Kusini. Makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha kwamba idadi ya watu wanaoishi mijini barani Afrika itaongezeka kwa milioni 953 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya karne hii, wakati maeneo ya miji barani Asia yataongezeka kwa zaidi ya watu bilioni mbili.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS

Mhariri : Othman Miraji