1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine kutoivamia kijeshi Crimea

12 Machi 2014

Rais wa mpito wa Ukraine, Oleksandr Turchynov amesema nchi yake haitalitumia jeshi lake kuizuia Crimea kujitenga, ili kuepukana na hatua ya kuuweka hatarini mpaka wake wa mashariki.

https://p.dw.com/p/1BNmb
Rais wa Mpito wa Ukraine, Oleksandr Turchynov
Rais wa Mpito wa Ukraine, Oleksandr TurchynovPicha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Turchynov alitoa kauli hiyo jana (11.03.2014), baada ya bunge la Crimea kupiga kura ya kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Ukraine kabla ya kura ya maoni kama Crimea ijiunge na Urusi, iliyopangwa kufanyika siku ya Jumapili.

Kiongozi huyo wa mpito amesema kitendo cha kuivamia kijeshi rasi hiyo ya Bahari Nyeusi, ambako majeshi ya Urusi yamechukua udhibiti, kutaiacha Ukraine inajulikana katika mpaka wake wa mashariki, ambako amesema Urusi imeweka meli zake za kivita.

Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk
Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy YatsenyukPicha: DW/ B. Riegert

Turchynov amesema Urusi inawachokoza ili waweze kuanzisha operesheni ya kijeshi katika eneo la Crimea, lakini hawatofanya hivyo kwa sababu Ukraine haitolindwa.

Kura hiyo ya maoni imeandaliwa na viongozi wa Crimea ambao hawatambuliwi na serikali mpya ya Ukraine inayoungwa mkono na Ulaya, ambayo iliingia madarakani baada ya maandamano ya miezi mitatu, yaliyosababisha vifo vya watu 100 na kumuondoa madarakani Rais Viktor Yanukovych anayeungwa mkono na Urusi.

Mataifa yenye nguvu duniani yamerejea wito wao kuitaka Urusi na Ukraine kutafuta suluhu ya mzozo huo, lakini Turchynov amesema viongozi wa Urusi wanakataa kushiriki katika mazungumzo ya aina hiyo.

Yatsenyuk aelekea Marekani

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk ameelekea Washington kwa mazungumzo na Rais Barack Obama wa Marekani, baadae leo (12.03.2014) kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa mataifa ya Magharibi na serikali ya Ukraine.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Yatsenyuk atautumia mkutano huo kutoa maelezo kuhusu umuhimu wa kupatiwa misaada ya kiuchumi. Ukraine inahitaji msaada wa Euro bilioni 35 kwa ajili ya kuiendesha nchi hiyo katika miaka miwili ijayo.

Jana baraza la Congress la Marekani, lilitaka Urusi ijiondoe haraka Ukraine na kumtolea wito Rais Obama kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, jana walishindwa kuondoa tofauti zao kwa lengo la kuutatua mzozo wa Ukraine.

John Kerry na Segei Lavrov
John Kerry na Segei LavrovPicha: Reuters

Mawaziri hao walizungumza kwa njia ya simu, bila kufikiwa kwa uamuzi kama Kerry akubali mwaliko wa kukutana na Rais Vladmir Putin wa Urusi mjini Moscow. Hata hivyo, Lavrov alimwambia Rais Putin kuwa Kerry ameukataa mwaliko huo, baada ya kuukubali hapo awali.

Mwadhishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman