1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

280610 EU USA SWIFT-Abkommen

29 Juni 2010

Umoja wa Ulaya na Marekani zimetilia saini makubaliano yatakayowaruhusu wachunguzi wa kimarekani kutumia taarifa za mabenki barani Ulaya katika mapambano dhidi ya ugaidi

https://p.dw.com/p/O5V8
Picha: EU

Makubaliano hayo yalitiwa saini mjini Brussels, na sasa yatafikishwa katika bunge la Ulaya kwa ajili ya kupigiwa kura kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Akizungumzia juu ya makubaliano hayo, mwanadiplomasia wa Marekani katika Umoja wa Ulaya, Michael Dodman amesema hiyo ni hatua muhimu kwa usalama wa Ulaya na Marekani.

Naye Kamishna anayehusika na masuala ya ndani katika Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstroem amesema ana matumaini makubaliano hayo mapya yataridhiwa na Bunge la Ulaya na kuanza kutumika tarehe mosi Agosti.

"Tuna matumaini kuwa wabunge watauridhia mkataba huu katika kikao chao wiki ijayo huko Strasbourg , na nnahakika kabisa kuwa hivi sasa wameyaelewa na kuyafahamu maboresho yaliyofanywa na kuwepo kwenye mkataba huu´´amesisitiza

Bunge hilo la Ulaya mwanzoni mwa February mwaka huu liliikataa rasimu ya awali ya makubaliano hayo. Wabunge wa bunge hilo walitumia kigezo cha kulinda haki ya masuala binafsi ya watu kuikataa rasimu hiyo.

Lakini kama anavyosema mbunge wa bunge hilo la Ulaya, anayetoka chama cha SPD hapa Ujerumani Birgit Sippel ni kwamba idadi kubwa ya wabunge wa upande wa Christian Democtrats, Social Democrats na waliberali wanaridhishwa na mpango huo mpya.

"Ulaya bado itakuwa na udhibiti katika maombi ya Marekani, iwapo kutadhihirika kuwepo kwa mshukiwa wa ugaidi na mwakilishi wa umoja wa Ulaya atakuwepo kuthibitisha hilo. Muhimu ni kwamba iwapo wakaazi wa Umoja wa Ulaya watahusika, hakutakuwepo na utaratibu wa kuwapeleka katika nchi nyingine nje ya Ulaya, kutegemeana na makubaliano ya nchi wanachama´´amesema

Kwa upande wake kiongozi wa kundi la wasoshalisti na mademokrat katika bunge hilo la Ulaya, Martin Schulz amesema, kilichobakia sasa ni kwa Marekani na Ulaya kushirikiana katika kuwalinda raia wake.

Hata hivyo amesema raia nao wana haki ya kulindwa na hatua za serikali kutaka kuingilia maisha yao kunakoweza kusababisha makosa.

Zaidi ya yote Umoja wa Ulaya unataka kuwa na mamlaka na uwezo mnamo kipindi cha miaka mitano ijayo, wa kupata taarifa za akaunti za watu mbalimbali. Mfumo unaotumika hivi sasa katika huduma za kifedha ambao ni mkubwa uitwayo SWIFT hautoi nafasi kwa hilo kufanyika.

Mwandishi:Christoph Prössl/Aboubakary Liongo/ZPR

Mhariri:Josephat Charo