1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wa kandanda unamwomboleza Cruyff

25 Machi 2016

Salamu ra rambirambi zinaendelea kutolewa kufuatia kifo cha nguli wa kandanda Mholanzi Johan Cruyff aliyefariki Dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 68 baada ya kuugua saratani ya mapafu

https://p.dw.com/p/1IJz0
Malaysia Fußball-Legende Johan Cruyff in Kuala Lumpur
Picha: Getty Images/M. Hewitt

Ilionekana kuwa hakuna ambaye angeweza kumzuia Johan Cruff. Sio mabeki mahiri wa miaka ya 70. Sio makocha wa timu pinzani wala wachambuzi. Sio hata ukosoaji wa mara kwa mara wakati wa nusu karne ambayo Cruyff alielezea mawazo yake – mara nyingi ya kushangaza, wakati mwingine ya ajabu na kuchekesha – kuhusu mambo ya kandanda. Kijanaa wa mitaa ya Amsterdam alikuwa na kipaji kilichoweza kumnyamazisha yeyote yule.

Ulimwengu wa kandanda umempoteza mmoja wa wanaspoti nguli aliyefariki Alhamisi mjini Barcelona akiwa na umri wa miaka 68 baada ya kuugua sraatani ya mapafu. Cruyff anasimama kando ya Pele, Diego Maradona na Franz Beckenbauer miongoni mwa wachezaji bora zaidi ambao mchezo huo umewahi kuwatengeneza. Watoto wengi walijaribu hata mpaka leo kuonyesha ujuzi wake, hasa “Cruyff turn“ mbinu aliyoitumia katika kuwapiga chenga na kuwaacha hoi mabeki. Andres Iniesta ni nahodha wa Barcelona "Natuma salamu za rambirambi zetu kwa familia na jamaa zake wote. Ni siku ya huzuni kwa kila mtu, sio tu kwa familia ya Barcelona, bali pia kwa familia ya ulimwengu wa kandanda ambao umeshuhudia mchango aliotoa kwa soka".

Fußball-WM '74 Niederlande - Argentinien 4:0 Johann Cruyff
Cruyff alikuwa na ujuzi wa kuwachenga na kuwaacha hoi mabeki wa timu pinzani upinzaniPicha: picture-alliance/dpa

Akiwa katika timu ya taifa ya Uholanzi, Cruyff aliucheza mfumo uliolibadilisha kandanda uliojulikana kama “kandanda kamili“ ambapo wachezaji walibadilishana nafasi zao, kwa kumsakama mpinzani kote uwanjani na kutamba kwa mtiririko wakiudhibiti mpira na pasi fupifupi. Mfumo ambao timu pinzani zilianza kuiga miaka iliofuata.

Alishinda mataji matatu ya ubingwa wa Ulaya akiwa na Ajax kuanzia mwaka wa 1971 hadi 1973. Alikuwa mchezaji bora wa mwaka Ulaya mara tatu na akatangazwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya katika karne ya 20. Aliisaidia Uholanzi kufika katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka wa 1974 ambayo Ujerumani ilishinda 2-1.

Baada ya kutoka Ajax, Cruyff alihamia Barcelona mwaka wa 1973 na aliisaidia klabu hiyo iliyokuwa katikati ya msimamo wa ligi kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza kwa karibu muongo mmoja. Baadaye kama kocha, aliingia katika mioyo ya mashabiki wa Barca aliposhinda Kombe la Ulaya mwaka wa 1992. Josep Bartomeu ni Rais wa Barca "siku zite tutamshukuru Johan. Alileta mabadiliko na filisofia mpya kwa soka. Alikishawishi kizazi kizima cha soka. Bila Johan Cruyff, Barca kama ilivyo sasa isingelieleweka".

Kabla ya hapo aliifunza Ajax na kushinda Kombe la 1987 la washindi wa ligi kuu za Ulaya. Kama tu walivyokuwa wenzake katika enzi hizo, Cruyff alikuwa mvutaji mkubwa wa sigara kama mchezaji na hata baada ya hapo. Aliwacha kuvuta sigara baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mwaka wa 1991. Na akaanzisha kampeni ya kupinga uvutaji sigara.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu