1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi mkali kabla G-8

23 Mei 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wameshughulishwa zaidi na hatua za ulinzi mkali kabla mkutano wa kilele wa G-8 na pia madhambi ya doping katika mashindano ya mbio za baiskeli .

https://p.dw.com/p/CHSt

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii, umeegemea zaidi mada 2:mjadala motomoto kuhusu hatua za usalama zilizochukuliwa na serikali kabla ya mkutano wa kilele wa dola kuu 8 tajiri(G-8) na hali ilivyo baada ya kuibuka visa vingi vya wendambio-za-baiskeli kuungama kuwa wakitumia madawa ya kutunisha misuli-doping.

“Katika dola inayofuata sheria ni sehemu ya jukumu la vikosi vya ulinzi kuchukua hatua na mapema kama iwezekanavyo kuwadhibiti wale wanaotaka kuzusha fujo na ambao wanataka kuitumia vibaya haki ya kuandamana kwa amani.

Kabla ya mkutano huo wa kilele wa dola kuu 8 za kiviwanda-G-8 huko Heiligendamm,Ujerumani, idara za usalama zimetumia barabara mamlaka yao kuzuwia fujo.Mashtaka kwamba, kwa kufanya hivyo zinataka kuwafanya wanaopanga kuandamana wahalifu, ni kuwasingizia nia mbaya.Yule ambae bado ana shaka shaka kwamba vikundi vyenye siasa kali vimejiwinda kufanya machafuko kwa kuandamana ,anapaswa kusoma ripoti za polisi.”

Ama MANNHEIMER MORGEN linatoa hoja sawa na hizo linapoandika:

“Demokrasia imara haihitaji kujikinga kwa waya za senyenge.Hatahivyo, inapaswa pia kuchukua hadhari ya kujilinda na wale ambao hawaheshimu kanuni za kidemokrasi.Dola linalofuata sheria hapa linabidi kupima uzuri na kuweka mezani ,kwani nani anaetaka kudiriki kuona wapinzani wa mkutano huo wa kilele kuhujumu kituo cha mkutano huo ?”

Nalo Hannoversche NEUE PRESSE likiendeleza mbele mada hii hii, lasema:

“Wanapokutana viongozi wenye nguvu kabisa wake kwa waume ili kuzingatia mustakbala wa dunia hii,wababidi pia kujiwinda kukabili malalamiko.Kujilinda nyuma ya uwa za waya wa senyenge na kupiga kwa madiri kubwa marufuku kwa maandamano si jambo linalokubalika.”

Gazeti la REUTLINGER-ANZEIGER laandika kuwa, hatua kali za kinga zilizochukuliwa zakumbusha enzi za GDR-Ujerumani Mashariki :Lalalamika:

“Kipimo kikubwa cha hatua zlizochukuliwa kuweka usalama zinamtia mtu wasi wasi,kwani zinakumbusha vitimbi kama hivyo vilivyokuwa vikitumiwa na Idara ya Usalama ya iliokua Ujerumani Mashariki (STASI).Ikiwa viongozi wa dola zenye nguvu ulimwenguni wakijitenga namna hivyo wasiguswe na ikihitajika vikosi vingi vya usalama kuwapo kuwalinda ili waweze tu kuzungumza bukheri-mustarehe-hii yaonesha tofauti kubwa iliopo kati ya watawala na watawaliwa.”

Mada ya pili iliochambuliwa leo kwa mapana na marefu katika magazeti ya Ujerumani na safu za wahariri, ni madhambi ya doping-matumizi ya madawa kutunisha misuli katika mbio za baiskeli.Muendesha-baiskeli maarufu Bert Diez na mwenzake Christian Henn, wamefichua jungu kubwa la madhambi hayo yaliofanywa siku za nyuma.

Gazeti la NORDBAYERISCHE KURIER linahisi:

“Spoti ya wendambio-za baiskeli imeambukizwa mno na madawa ya kutunisha misuli.Yule asiejipiga sindano kuongeza nguvu mwilini au asiemeza vidonge, hana nafasi ya ushindi.Lakini ni pale tu mbio za baiskeli zitakapojikomboa na madhambi haya ya doping,ndipo zitakapoweza kufungua ukurasa mpya.Kwani, kilicho hatarini hapa, ni hatima ya mashindano ya baiskeli.Kwani, mashabiki wake wanazidi kufadhahika na wakati sasa umewadia uchafu huu kufagiliwa barabara ili mashindano yam bio za baiskeli yabaki hayi.”