1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi umeimarishwa katika eneo la Jisr al Shangour

10 Juni 2011

Jeshi nchini Syria limeanza operesheni za kurejesha usalama katika eneo la kaskazini magharibi la Jisr al Shangour, karibu na mpaka wa Uturuki, huku wanaharakati wa demokrasia wakiapa kuendelea na maandamano

https://p.dw.com/p/11Y3u
Waandamanaji nchini Syria wanaopinga utawala wa rais Bashar al AssadPicha: AP

Hayo yanajiri huku Waziri mkuu wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, ameushtumu utawala wa Syria kwa kufanya ukatili dhidi ya waandamanji wanaoipinga serikali.

Serikali ya Syria imesema operesheni hiyo imejiri baada ya wakaazi wa Jisr al Shunguor kutoa mwito wa kupewa ulinzi, baada ya serekali kusema polisi120 waliuwawa na magenge ya watu waliojihami mapema wiki hii. Televisheni ya kitaifa nchini humo imesema katika kuitikia mwito wa wananchi, vikosi vya jeshi vimeanza misako yake katika mji huo ili kuwakamata watu waliojihami. Iliongeza kuwa makundi ya watu waliojihami yaliteketeza moto viwanja karibu na mji huo wa Jisr al Shungour , ambao ni sehemu ya mkoa wa Idlib.

Mjini Geneva kamishna wa haki za binadam wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema wanaharakati wanasema takriban watu 10,000 wametiwa mbaroni kufikia sasa.

Inaripotiwa kuwa operesheni hiyo kubwa ya kijeshi dhidi ya wapinzani wa serikali inawahusisha wanajeshi 30,000. Serikali ya syria inasema magaidi na majangili waliwashambulia wanajeshi na kujaribu kuliteka eneo hilo, Lakini wanachama wa upinzani wanasisitiza kuwa vifo hivyo vilikuwa vya wanajeshi waliouwawa na wenzao katika tukio la uasi. Baada ya serikali ya syria kuapa kulipiza kisasi mauaji ya wanajeshi wake 120, zaidi ya wasyria 2,400 wamekimbia eneo hilo karibu na mpaka na kuingia Uturuki katika siku za hivi karibuni kwa hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Türkei Ministerpräsident Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan, rafiki wa karibu wa AssadPicha: dapd

Hayo yanajiri wakati Waziri mkuu wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, akiushtumu utawala wa Syria kwa kufanya maovu dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali, nayo ufaransa ikiishtumu kwa mauaji ya halaiki. Upinzani umeitisha maandamano zaidi hii leo yanayoítwa..“ijumaa ya mshikamano wa makabila“, ukitumia ukurasa wa facebook kueneza mwito wao.

Erdogan ameongeza shinikizo dhidi ya Assad, rafikiye wa karibu, kuanzisha mageuzi japo hajamtaka ajiuzulu. Televisheni ya Uturuki Annatolia imemnukuu waziri mkuu huyo akisema alizungumza na Assad siku nne au tano zilizopita, lakini akaipuuza hali hiyo. Anasikitika kuwa syria haiishughulikii vyema hali hiyo ambayo amesema ni ukatili mkubwa.

Katika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, mataifa ya magharibi yameanza kujadili azimio lililowasilishwa na Uingereza na Ufaransa wanaotaka kusitishwa ghasia na kuwekwa marufuku ya silaha nchini Syria.

Zaidi ya watu 1,300 wameuwawa nchini Syria tangu maandamano ya kumpinga rais Bashar al Assad yalipoanza mwezi machi. Haya ni kwa mujibu wa makundi ya wanaharakati.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Miraji Othman