1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaarufu wa Rais Obama wadidimia

29 Oktoba 2014

Rais wa Marekani Barack Obama pamoja na chama chake cha Democratic, wanakabiliwa na changamoto ya kupoteza viti vya Baraza la Seneti la Marekani katika uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika tarehe 4 Novemba.

https://p.dw.com/p/1Ddf0
Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: Reuters/G. Cameron

Uchaguzi huo wa katikati ya muhula, ni wa viti vyote 435 vya Baraza la wawakilishi na viti vipatavyo 33 vya baraza la Senete lenye jumla ya viti 100.

Kutokana na kupoteza umaarufu kama kiongozi bora kwa wananchi wake, Rais Obama inasemekana atashidwa kusaidia chama chake cha Democratic kupata ushindi wa viti vya Baraza la Seneti. Wengi wa wajumbe wa chama hicho wanaonekana wakimkwepa Rais Obama ili hali yake ya kupungukiwa na ungwaji mkono isiathiri kampeni zao.

Seneta wa chama cha Democratic Mark Begish, amesema Rais Obama kuwa hana umuhimu tena kwa vile ataondoka madarakani baada ya miaka miwili.

Ishara nyengine ya jinsi gani wagombea wa chama cha Democratic wanajivuta mbali na Rais Obama, ni kutoka kwa mgombea wa jimbo la Kentucky Alison Grimes, ambaye katika mjadala hivi karibuni alikataa hata kusema kama alimpigia kura rais huyo katika uchaguzi uliopita.

Obama alivutia umati mkubwa wakati wa kampeni yake ya mwisho ya mwaka 2012, lakini sasa miaka miwili baadae inaonekana wazi kuwa Rais huyo amepoteza mvuto kwa wananchi wa Marekani na atalazimika kukaa mbali na mikutano ya kampeni muhimu za viti vya Baraza la Seneti ambazo zimebakiwa na mwezi mmoja tu hadi kuanza kwa uchaguzi.

Katika kampeni za televisheni zinazoendelea huko Marekani, chama cha Republican kinawalaumu wagombea wa chama cha Democratic kwa kumpigia kura rais huyo miaka miwili iliyopita.

"Jina langu halipo kwenye sanduku la kura, bali ni ni maadili yetu na yale ya vizazi vilivyopita waliopigania taifa letu liwe ni mahala pa haki sawa na mafanikio" alisema Obama akizungumza na kundi la wafadhili mapema mwezi huu.

USA Anschlag Boston Marathon Explosion Reaktionen Trauer Capitol Hill
Jengo la Bunge la Marekani, mjini Washington, DCPicha: Getty Images

Mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi Marekani

Ingawa uchaguzi huo utakuwa wa Baraza la Seneti pamoja na Baraza la wawakilishi, lakini kiasi ya asilimia ya 32 ya wapiga kura wanasema kuwa kura zao ni ujumbe wa kumpinga rais Obama.

Kiujumla mazingira ya kisiasa yanaonekana yakiegemea zaidi chama cha Republican, na huku maseneti wa chama cha Democratic waliopata madaraka kufwatia ushindi wa mwanzo wa rais Obama wa mwaka 2008, wanakabiliwa na changamoto nyingi katika majimbo ya kihafidhina ambayo ndio makaazi ya wafuasi wengi wa chama cha Republican, chenye siasa za wastani za mrengo wa kulia.

Chama cha Republican kitahitaji kupata viti sita ili kuweza kukipokonya udhibiti wa baraza la seneti chama cha Democratic. Warepublican wana uhakika wa kunyanyakuwa majimbo matatu ya South Dakota West Virginia na Montana.

Kwa mujibu wa mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Virginia Larry Sabato, kuna mategemeo makubwa ya ushindi wa chama cha Republican labda chama hicho kipatwe na bahati mbaya, aliengeza kuwa ushindi kwa chama hicho upo wazi

Katika ripoti ya kituo cha utafiti cha Pew iliyotoka mwezi mmoja uliopita ilisema kwamba, asilimia 15 tu ya wamarekani wanafwatilia kwa karibu uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika tarehe 4 Novemba, lakini wengi wao wanafuatilia zaidi habari zinazopazwa katika vyombo vya habari, juu ya makundi ya kigaidi ya itikadi kali za kidini pamoja na ugonjwa wa Ebola.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman