1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaru Yar ´Adua aongoza

Josephat Charo23 Aprili 2007

Mjadala mkubwa umezuka kufuatia uchaguzi uliofanyika juzi Jumamosi nchini Nigeria. Vyama vya upinzani nchini humo vimetangaza havitayakubali matokeo ya uchaguzi huo huku tume ya uchaguzi ya Nigeria ikiusifu kuwa wa kihistoria.

https://p.dw.com/p/CHFh
Mgombea urais wa chama tawala nchini Nigeria Umaru Yar ´Adua
Mgombea urais wa chama tawala nchini Nigeria Umaru Yar ´AduaPicha: AP

Mgombea urais wa chama tawala nchini Nigeria, Umaru Yar ´Adua, anaongoza kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchaguzi wa Nigeria huku uchaguzi huo ukikosolewa vikali.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Nigeria, Maurice Iwu, jana alisema uchaguzi nchini humo ulifanyika kwa njia huru na ya haki. Aidha bwana Iwu alisisitiza kuwa uchaguzi huo utakuwa tukio muhimu katika historia ya Nigeria.

´Hakujatokea matukio yoyote makubwa ingawa katika baadhi ya vituo, upigaji kura ulianza kuchelewa na tukaruhusu uendelee. Uchaguzi kwa kiwango kikubwa umefaulu. Tumefaulu na hatujawahi kufikia ufanisi huu. Sisi ni nchi inayojivunia na ni watu wenye furaha.´

Mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi alisema ililazimu uchaguzi uchelewa katika baadhi ya vituo kwa sababu mahakama kuu ya Nigeria iliamua mnamo Jumatatau tarehe 16 mwezi huu kumruhusu makamu wa rais, Atiku Abubakar, kugombea wadhifa wa urais. Hata kabla uamuzi huo wa mahakama bwana Iwu alisisitiza uchaguzi haungechelewa.

Mwenyekiti wa shirika kubwa la waangalizi wa uchaguzi liitwalo Transition Group, bwana Innocent Chukwuma, jana aliukosoa uchaguzi nchini Nigeria akisema ulichelewa katika baadhi ya vituo na vituo vya kupigia kura vilikosekana katika maeneo kadhaa.

´Hayo yote yakijumulishwa pamoja hayaufanyi uchaguzi kuwa halali. Tulishuhudia hayo mwaka 1999 na mwaka 2003. Swali sasa ni je tunatakiwa kuendelea na aibu hii kwa sababu ya uchaguzi au kuamua kufanya uchaguzi wa haki? Hiyo ndio sababu tunayakataa matokeo ya uchaguzi wa tarehe 21 Aprili.´

Atiku Abubakar ameuleza uchaguzi wa Nigeria kuwa mbaya zaidi kuwahi kufanyika nchini humo. Alisema atakutana na wagombea wengine wa upinzani kujadili hatua watakayochukua. ´Imani yetu iko katika mahakama nchini humu. Hilo ndilo tumaini letu la pekee.´

Waangalizi wa kimataifa wana wasiwasi ikiwa matokeo ya uchaguzi wa Nigeria yanaashiria uamuzi wa Wanigeria. Kundi la waangalizi 17 wa jumuiya ya madola, Commonwelath, jana liliipongeza tume ya uchaguzi ya Nigeria kwa kuboresha usalama na maandalizi ya uchaguzi huo. Lakini kiongozi wa ujumbe wa Commonwelath, bwana Joseph Warioba, kutoka Tanzania hakutaka kutoa tathmini yake.

´Shughuli hii bado haijakamilika. Tumeshuhudia upigaji kura lakini kuna kazi nyengine inayoendelea hasa kukusanya, kuhesabu na kutangaza matokeo. Tunazuia maamuzi yetu hadi tutakapoyachunguza.´

Rais mpya wa Nigeria anatarajiwa kutangazwa hii leo huku wasiwasi ukizidi katika ngazi za kimataifa kuhusu uchaguzi wa Jumamosi iliyopita. Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake juu ya matukio yasiyo ya kawaida na machafuko wakati wa uchaguzi huo. Umesema Wanigeria wengi hawakuwa huru kupiga kura bila hofu.

Ripoti ya mwisho ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya itachunguza uchaguzi wa rais na ofisi ya rais wa Umoja wa Ulaya imeitaka serikali ya Nigeria isema ukweli kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.