1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika watimiza nusu karne

24 Mei 2013

Umoja wa Afrika unatimiza miaka 50 tangu kuundwa kwake hapo tarehe 25 Mei 1963 kwa jina la Umoja wa Nchi Huru za Afrika kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni na kumaliza utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini.

https://p.dw.com/p/18ckK
A banner is held aloft above black students in Johannesburg, South Africa, in the township of Soweto where they rallied after the funeral of a 16-year-old black student who died in jail, Oct. 18, 1976. The student, Dumisani Mbatha, who was arrested following a protest march last month by young blacks in Johannesburg, died two days after his arrest Sept. 23. (AP Photo)
Bildergaleries 50-jährige Jubiläum der Afrikanischen Union AUPicha: AP

Tokea mabadiliko ya kidemokrasia katika Rasi ya Matumaini Mema na kumalizika vita baridi, Umoja huo unatafuta njia za kuwa na msimamo wake wenyewe. Unalenga kuleta ushirikiano wa kikanda, kuondoa vizuizi vya lugha na biashara na hatimaye siku moja kuleta muungano wa bara zima la Afrika.

"Mtukufu Mfalme, mwenyekiti, waheshimiwa wenzangu, ndugu na marafiki: Kwa hakika ile hali ya viongozi 32 kukusanyika hapa Addis Ababa ni ushahidi wa wazi wa haja kubwa waliyonayo raia wetu baada ya uhuru. Bara zima limetupa mamlaka ya kuwa na mkutano huu chini ya msingi wa Umoja wetu." Maneno hayo yalitamkwa tarehe 25 Mei 1963, mjini Addis Ababba, Ethiopia kwenye hotuba ya kusisimua Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah, juu ya kibali cha kuundwa kwa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU). Lengo la pamoja: Umoja wa bara hilo , lenye nguvu kiuchumi na uhuru wa kisiasa.

Mwanzo wake

Miaka sita kabla ya hapo, muasisi Nkurumah kutoka kile kilichokuwa kikijulikana kama koloni la Uingereza "Pwani ya Dhahabu", leo hii Ghana, aliiongoza nchi hiyo kuwa huru na akawa ndiye baba wa vuguvugu la uzalendo wa Mwafrika katika kuliongoza jukwaa la mataifa machanga kupambana dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.

Kwame Nkrumah
Kwame NkrumahPicha: Getty Images

Muongozo muhimu, ambao ni ule wa kutoingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine huru, ukageuka hatimae kuwa janga kwa Umoja huo, kwani mtindo wa mapinduzi ya kijseshi wa miaka ya 1960 na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipotokea, viongozi wa mataiafa ya Afrika walibakaia kimya wakiangalia .

Madai kwamba OAU ilishindwa wakati wote ni jambo linalopingwa na balozi wa zamani kutoka Ethiopia, Mengiste Desta. "Ninayapinga vikali madai kawamba OAU ulikuwa Umoja uliokosa meno ya kuuma. Kinyume ulikua na meno makali mno -ikiwa mtu atatambua malengo ya kuundwa kwake, yaani kulikomboa bara zima kutokana na ukoloni na sera ya ubaguzi wa rangi."

Hata hivyo muda si mrefu ulishinddwa kutimiza fikara ya awali, anasema Dr Mehari Maru, mtaalamu wa masuala ya Umoja wa Afrika kutoka Taasisi ya Masuala ya Usalama (ISS), mjini Addis Ababa. "Kumalizika kwa ukoloni na sera ya ubaguzi wa rangi, kulifungua njia ya kuwepo mjadala. Nini maswala mapya ya Umoja huo na kutokana na hayo pakahitajika taasisi mpya kuleta mabadiliko yanayohitajika na hivyo ukaazaliwa Umoja wa Afrika."

Umoja wa Afrika

Baada ya kuupa jina jipya la Umoja wa Afrika (AU) ambao uliundwa 2002 mjini Durban, Afrika ya Kusini, baada ya kumalizika vita baridi, madhumuni yake yakawa ni kuleta muungano wa kiuchumi na demokrasaia.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/ dpa

Kiroja cha mambo katikati ya miaka ya 1990, kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi aliyejitangaza "Mfalme wa Wafalme" wa Afrika, alilazimisha fikra ya mtazamo wa Nkrumah wa "Muungano wa Afrika,", ingawa ilikuwa siasa kwa masilahi ya kisiasa ya Gaddafi kuliko kuwa hatua ya kifalsafa.

Hata hivyo, mpango wake wa kuwa na jeshi moja, sarafu moja, biashara na kusafiri bila vizuizi kama ilivyo katika Umoja wa Ulaya ulisababisha mgawanyiko zaidi kuliko umoja. Kutokana na mvutano huo kukazuka kambi mbili na Afrika ya Kusini yenye nguvu kisiasa ikasimama kumpinga Gaddafi.

"Bila shaka matokeo kwetu si ya kuridhisha. lakini tunasonga mbele pamoja na nina hakika siku hadi siku tutafikia karibu lengo la "Muungano wa Afrika." Alisema mjumbe wa Gaddafi kwenye Umoja huo, baada ya kuvunjwa moyo na kile alichokiona ni udhaifu, aliwaambia wajumbe baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2009. Gaddafi mara kwa mara alikuwa akitowa matamshi makali kwa waliompinga kwa kuzingatia kile alichokiona ni mapenzi ya Waafrika wengi kwake.

Hatimaye

Ingawa wazo hilo lilizusha mabishano na kutoa sura ya mgawanyiko miongoni mwa mataifa, Umoja wa Afrika sasa una waziri wa ndani wa Afrika ya Kusini Nkosazana Dlamini-Zuma kama Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo, mwana mageuzi aliyetangaza haraka kwamba anataka kuona unawajibika zaidi. Halmashauri hiyo kuu inataka kuendeleza sera ya kuadhibu kwa kusimamisha uanachama na vikwazo kwa wanaokiuka katiba na muongozo wake.

Picha ya tarehe 25 Mei 1963 siku ya kuundwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika.
Picha ya tarehe 25 Mei 1963 siku ya kuundwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika.Picha: STR/AFP/Getty Images

Mtihani kwa uwajibikaji na nguvu za kiutendaji za Umoja wa Afrika, kandoni mwa pigo la ujumbe wake wa AMISOM nchini Somalia, ni mgogoro katika mataifa ya Afrika ya Magharibi ya Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kwa Maoni ya Mehari Maru kutoka Taasisi ya Masuala ya Usalama ni kwamba "Leo Afrika ni ya kidemokrasia zaidi kuliko miaka kumi iliyopita ambapo tulikuwa na serikali chache zilizochaguliwa kidemokrasia. Lakini hili halipaswi kutafsiriwa kwamba ni uongozi wa kidemokrasi. Demokrasia ni kutambua fikra tafauti, kwani ndiyo msingi wa matatizo ya kisiasa Afrika."

Sherehe za Jumamosi

Katika Sherehe za Jumamosi, miongoni mwa mambo mengine ni mchuano wa kandanda kati ya wanachama waasisi Ethiopia na Sudan. Pia Umoja huo unasherehekea pamoja na Ujerumani, kwa sababu tangu miaka kadhaa, Ujerumani imekuwa ikiliiunga mkono Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa kusaidia mafunzo.

Sherehe za miaka 50 ya Umoja wa Afrika.
Sherehe za miaka 50 ya Umoja wa Afrika.Picha: AFP/Getty Images

Afisa anayehusika na masuala ya Afrika katika Wizara ya mambo ya nchi za nje mjini Berlin, Egon Kochanke, anazungumzia mustakbali mwema akisema kwamba malengo waliyokuwa nayo Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, na Kwame Nkrumah wa Ghana miaka 50 iliopita, yalikuwa ni kuleta maendeleo ya kisiasa na kiuchumi barani Afrika na kuwa na mtazamo wa pamoja kuweza kuyafikia. Kidogo mafanikio si kama yalivyotarajiwa, lakini leo hii Umoja wa Afrika una nguvu na msimamo wenye nguvu sana katika sera ya kigeni na usalama na pia upigaji kura."

Miaka 50 ya Umoja wa nchi huru za Afrika sasa Umoja wa Afrika, bara hilo limezindukana zaidi. Wakati Rais wa Ujerumani Joachim Gauck alipozuru Addis Ababa hivi karibuni na kupendekeza kuongezwa mchango wa wanajeshi wa Ujerumani, hilo halikupata shauku kutoka kwa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Dlamini-Zuma. Kauli mbiu ya " Suluhisho la matatizo ya Afrika ni la Waafrika wenyewe," inapewa kipaumbele miaka 50 mengine ijayo ndiyo itakayotowa jibu.

Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Mohamed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohammed Khelef