1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuingilia kati Jamhuri ya Afrika ya kati

Hahn, Julia5 Desemba 2013

Wakati baraza ya la usalama la usalama la Umoja wa Mataifa likitizamiwa kuiruhusu Ufaransa kupeleka vikosi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, hali nchini humo inazidi kutia wasiwasi kutokana na ongezeko la machafuko.

https://p.dw.com/p/1ATL8
Picha: Reuters

Jamhuri ya Afrika ya Kati inakabiliwa na kitisho cha kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ripoti za vyombo vya habari zinaelezea kukithiri kwa vitendo vya ubakaji, mateso, mauaji ya hovyo na pia vurugu za kidini. Tangu mwezi Septemba, mapigano kati ya Waisalmu wa Wakristu yamewaua watu wasiopungua 150, na katika maeneo mengi silaha na mapanga vimezagaa.

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Michell Djotodia.
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel Djotodia.Picha: STR/AFP/Getty Images

Ufaransa yataka kupeleka wanajeshi 1000
Ufaransa ilitangaza wiki iliyopita kwamba ingetuma wanajeshi 1000 zaidi katika taifa hilo lenye migogoro, ili kusaidiana na vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyopo nchini humo, MISCA. Hata hivyo hatua ya Ufaransa ilikuwa haijapata baraka za baraza la usalama, na inatarajiwa kwamba baraza hilo litaidhinisha muswada wa azimio la Ufaransa katika chake cha leo Alhamisi. Azimio hilo linapendekeza kuwekwa viwazo vya silaha, na kuutaka Umoja wa Mataifa kufikiria kukigeuza kikosi cha Umoja wa Afrika kuwa cha Umoja wa Mataifa.

Thierry Vircoulon, Mkurugenzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kundi la kushghulikia migogoro la International Crisis Group, anasema ipo haja ya kuingilia haraka kunusuru hali ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati: "Hali ni mbaya na ya kutisha sana hasa katika mji wa Bangui. Huko jambo dogo sana linaweza kusababisha moto mkubwa. Taifa hili liko katika hali ya machafuko."

Mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ulisababishwa na kuangushwa kwa utawala wa rais wa zamani Francois Bozize na kundi la waasi wa Seleka, ambao wengi wao ni Waislamu. Rais wa sasa, Michell Djotodia, alichukua uamuzi wa kulivunja kundi hilo mwezi Septemba, lakini wapiganaji wa zamani wa kundi hilo wanadaiwa kuendelea kufanya vurugu.

Makundi yanayohisi usalama wao unatishiwa yalijipanga na kuunda vikundi vya kujilinda maarufu kama anti-balaka, na wakati mwingine vikundi hivi vimekuwa vikiwashambulia Waislamu, ambapo katika tukio lililotokea Jumanne wiki hii, watu wasipoungua 12 waliuwa na watu wanaodaiwa kutoka katika kikundi cha anti-balaka. Tayari Marekani na Ufaransa zilionya katikati mwa mwezi Novemba juu ya kutokea mauaji ya halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius akiwa na waziri mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Nicolas Tiangaye.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius akiwa na waziri mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Nicolas Tiangaye.Picha: Pierre Andrieu/AFP/Getty Images

Kuingilia kijeshi tu hakutoshi
Rais wa shirika la misaada la Madaktari wasio na mipaka nchini Ufaransa MSF, Mego Terzian anasema ni mapema mno kutumia neno mauaji ya halaiki, lakini anakiri kuwa hali ni mbaya, na kwamba shirika lake linafuatilia hali, hasa kaskazini na katikati mwa taifa hilo, ambako vurugu zinatokea mara kwa mara. Pamoja na hayo, Terzian anasema idadi ya wanajeshi 1000 ambao Ufaransa inataka kuwapeleka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati haitoshi kabisaa.

Terzia anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia serikali ya jamhuri ya Afrika ya Kati, kujenga upya miundombinu na kurejesha utawala wa sheria nchini humo. Hivi sasa mamia ya raia wanaotoroka vurugu katika maeneo mengi, hujikuta wakiishi maporini kwa wiki kadhaa. Umoja wa Mataifa nao unaonya juu ya kutokea baa kubwa la njaa wakati ambapo karibu watu milioni moja hawako katika nafasi ya kuweka chakula mezani.

Mwandishi: Köpp Dirke
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman