1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waitaka Mali kufanya uchaguzi Februari

Daniel Gakuba
25 Oktoba 2021

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.

https://p.dw.com/p/429GQ
Mali - Delegation des UN-Sicherheitsrats in Bamako
Picha: Présidence de la République du Mali

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao uliizuru Mali kutathmini hali ya usalama, umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.

Wito huo utawezesha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS baada ya mapinduzi ya mwaka uliopita.

Ujumbe huo ulioongozwa na Balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, mwishoni mwa juma ulikutana na wadau muhimu katika makubaliano hayo.

Ujumbe wa UN umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.
Ujumbe wa UN umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.Picha: Présidence de la République du Mali

Akizungumza na waandishi habari hapo jana mjini Bamako, Balozi Kimani amesema wameguswa na matakwa ya wananchi wa Mali kuhusu mageuzi ya kisiasa na kikatiba na kwa sasa wanasubiri kumalizika kwa kipindi cha mpito ambacho kinapaswa kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi.

Hata hivyo  viongozi wa mpito wa Mali wamesema watathibitisha tarehe ya uchaguzi baada ya kufanyika mazungumzo ya mwezi Desemba miongoni mwa makundi yanayohusika.