1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wakataa ombi la Kenya kuhusu ICC

Admin.WagnerD24 Mei 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelikataa ombi la Kenya la kutaka kufutiliwa mbali kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika mahakama ya ICC kutokana na ghasia za mwaka 2008.

https://p.dw.com/p/18dKk
Picha: Getty Images

Ombi hilo la Kenya kwa mara nyingine limepingwa vikali na mataifa ya magharibi katika baraza hilo la usalama lenye wanachama 15 na kuwaambia viongozi hao wa Kenya katika kikao cha faragha kuwa sharti wakabiliwe na mashitaka hayo katika mahakama ya ICC.

Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, Macharia Kamau, baada ya mkutano huo wa faragha amesema Kenya imetaka kesi hizo kusitishwa haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa jinsi zitakavyositishwa na nani atakayezitisha hilo ni suala jingine lakini bila shaka zinahitaji kutupiliwa mbali kwani zinatatiza amani na haki nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta, naibu wa Rais William Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa madai ya kuhusika katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 ambazo zaidi ya watu 1,000 waliuawa. Wote watatu wamekanusha madai hayo.

Rais wa Kenya Uhuru na naibu wake Ruto
Rais wa Kenya Uhuru na naibu wake RutoPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kesi dhidi ya Kenyatta imepangiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu na ameahidi kushirikiana na mahakama ya ICC, lakini wakati huo huo akifanya kampeini kabambe dhidi ya kesi hiyo.

Kenya yazirai nchi za Afrika kuiunga mkono

Kulingana na hati za Umoja wa Afrika, Kenya inazirai nchi nyingine barani Afrika kuishawishi mahakama ya ICC kutupilia mbali kesi dhdi ya viongozi hao. Nchi nyingi za Afrika ni wanachama wa mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo ya kimataifa, lakini kumekuwa na mashaka miongoni mwa mataifa hayo kuwa ICC inawalenga viongozi wa Afrika pekee katika kesi zake.

Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini leo amesema nchi yake haiwezi kuwa mwanachama wa ICC, kwani mahakama hiyo inakusudia tu kuwakandamiza viongozi wa Afrika.

Hati iliyowasilishwa kwa mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika katika kikao cha Umoja wa Afrika kinachokutana nchini Ethopia imetaja kuwa mahakama hiyo inahatarisha uthabiti wa Kenya wakati nchi hiyo inapofanya mageuzi makubwa ili kuepuka kutumbukia tena katika ghasia kama za miaka mitano iliyopita na kuzihimiza nchi za Afrika kuitaka ICC kusitisha kesi hizo au kuzirejesha nchini Kenya.

Viongozi wa Afrika
Viongozi wa AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Rais Uhuru Kenyatta ndiye kiongozi wa pili wa Afrika aliye madarakani kukabiliwa na kesi katika mahakama hiyo baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi Machi mwaka huu.

Marais wawili wa Afrika wana kesi ICC

Rais wa Sudan Omar al Bashir pia anatakiwa kujibu mashitaka katika mahakama hiyo ya ICC kwa uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki licha ya kuwa nchi yake si mwanachama wa mkataba wa Roma.

Marekani ambayo pia si mwanachama wa mahakama hiyo ikishirikiana na mataifa ya magharibi, imekuwa ikisisitiza kuwa viongozi hao wa Kenya hawana budi kujibu mashitaka yanayowakabili na kupinga juhudi zozote za kutupilia mbali kesi dhidi yao.

Rwanda, ambaye ni mwanachama asiye wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inaripotiwa kuwa nchi pekee kwenye baraza hilo iliyounga kutupiliwa mbali kwa kesi za ICC dhidi ya Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef.