Umoja wa Mataifa wamtaka Jenerali Haftar asimamishe mashambulio

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeyataka majeshi ya Jenerali muasi Khalifa Haftar yasiendelee na msafara wake kuelekea katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Balozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa Christoph Heusgen amelitaka jeshi hilo la jenerali Haftar liache pilikapilika zote za kijeshi. Balozi Heusgen amesema hayo baada ya kikao cha Baraza la Usalama mjini New York.

Kwa sasa Ujerumani ndio mwenyekiti wa Baraza hilo. Hapo awali mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za G 7 pia walitaka kukomeshwa kwa mapambano. Mawaziri hao wamesema mgogoro wa nchini Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya mapigano karibu na Tripoli ambayo wamesema yanaweza kuvuruga utulivu na matarajio ya usuluhishi wa Umoja wa Mataifa wa kuutatua mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Wanamgambo wanaoiunga mkono serikali magharibi mwa Libya walipambana na vikosi vya jenerali muasi Khalifa Hifter siku ya Ijumaa, na kuwateka askari wake 100. Majeshi ya serikali yalitumia ndege kushambulia ngome za jenerali Haftar muda mfupi baada ya jenerali huyo kuyaamuru majeshi yake kuelekea mjini Tripoli.

Mapambano hayo yalitokea wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipokuwa anamaliza ziara yake iliyokuwa na lengo kuepusha kuongezeka kwa mgogoro. Guterres  alikutana na jenerali Haftar kwenye mji wa Benghazi.

Mkutano wa kimataifa juu ya kuutatua mgogoro wa nchini Libya utafanyika baadae mwezi huu chini  ya udhamini wa Umoja wa Mataifa. Tangu kuondolewa madarakani kwa kanali Muammar Gaddafi Libya imegawanyika katika serikali mbili ya mashariki na ya magharibi pamoja na makundi mbali mbali ya wanamgambo.

Vyanzo: AP/p.dw.com/p/3GNljMaudhui Zinazofanana

Tufuatilie