1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wamtaka Nkunda asitishe hujuma

Kalyango Siraj30 Oktoba 2008

Nkunda akubali lakini aonya kuwa akichokozwa ataendeleza mapambano licha ya lawama

https://p.dw.com/p/FkK6
Wananchi maelfu kadhaa wakimbilia Goma kutoka sehemu za vitaPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulio yanayofanywa na waasi wa wanaoongozwa na Laurent Nkunda katika eneo la mshariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Mashambulio ya waasi yalikuwa yanaelekezwa mji wa Goma. Sasa waasi wanasema wamesitisha hujuma yao,lakini wakimbizi baado wanamiminika katika mji huo.

Kulaani kwa baraza hilo kunafuatia taarifa kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wanaoongozwa na Generali Nkunda walikuwa wanausogolea mji wa Goma ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.Baraza la usalama ambalo linawajumulisha wanachama 15 limemtaka Generali huyo kusitisha hujuma zake mara moja.

Na kama kuitikia mwito huo inasemekana waasi hao wamesitisha hujuma na kutaka mapigano ambayo yamedumu siku nne dhidi ya majeshi ya serikaliya Kinshasa yakomeshwe.

Generali Nkunda ameviambia vyombo vya habari vya nchi za magharibi kuwa amesitisha mapigano ili kuzuia wasiwasi katika mji wa Goma na kuviomba vikosi vya serikali kuitikia mwito wa kuweka chini silaha.Aidha amesema anataraji kuwa majeshi ya Umoja wa Mataifa ya MONUC yataweza kulinda mji huo ambao inasemekana kuwa umevurugwa na wanajeshi wa serikali wanaotoroka mapigano ambao inadaiwa wanaiba, na kufyatua risasi ovyo.Kamanda mmoja wa jeshi la serikali ya Kinshasa ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa takriban watu watano wamaeuwa.Lakini meya wa mji huo Roger Rashidi Tumbula ameiambia DW kwa simu kuwa waliuoawa na wanajeshi wanafikia 17.

Mji wa Goma ulikumbwa na wasiwasi jumatano wakati waasi waliposemekana kuwa walikuwa karibu kuuteka.Kanali wa jeshi la serikali Jonas Padiri akisema kuwa mji huo uko mikononi mwa vijana wake,lakini Laurent Nkunda amesema kuwa anataka kikosi cha MONUC kichukue dhamana ya kuulinda .Akizungumza na kituo kimoja cha Televisheni cha Ufaransa amedai kuwa wapiganaji wake walikuwa karibu na uwanja wa ndege wa Goma lakini akaamua kurudi nyuma ili kuondoa wasiwasi miongoni mwa wananchi wengi ambao wamekimbilia huko.

Kuhusu habari kuwa Ufaransa inaweza ikatuma wanajeshi wake huko Nkunda amesema kuwa jambo hilo si baya almradi hawatakuwa na upendeleo .Amesema kuwa ‚Ikiwa watakuja kwa lengo moja la kusaidia FDLR hatutawakaribisha bali tutapigana dhidi yao’

FDLR ni waasi wa Rwanda waliokimbilia Kongo baada ya kushutumiwa kuendesha mauaji ya halaiki.Serikali ya Rwanda ya sasa pamoja na waasi wa Nkunda wanailaumu serikali ya Kinshasa kwa kuwatumia FDLR katika mapigano dhidi ya kundi la Nkunda ambalo linawajumulisha watu wa kabila la wanyamulenge.

Utawala wa Kinshasa nao kwa upande wake unaulaumu utawala wa rais Paul Kagame kwa kumuunga mkono Nkunda kwa hali na mali.Madai hayo yamekanushwa na Nkunda pamoja na serikali ya Kigali. Shirika la habari la AFP linasema waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda, Rosemary Museminari,amekanusha madai ya kusaidia Nkunda wakati akizungumza na radio ya taifa ya Rwanda.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu laki mbili unusu wamekimbia mapigano tangu Agosti, na hilo kujumulisha idadi ya wakimbizi katika mkoa wa Kivu Kaskazini kufikia millioni moja.