1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali ya Afrika ya Kati

7 Januari 2014

Umoja wa Mataifa wameonya kuwa mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati unakaribia kuwa janga, huku nusu ya idadi ya watu wakiachwa bila makaazi tangu machafuko ya kimadhehebu yalipozuka

https://p.dw.com/p/1AmE3
Zentralafrikanische Republik Elend
Picha: Fred Dufour/AFP/Getty Images

Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltmasn ameliambia Baraza la Usalama kuwa karibu watu milioni 2.2 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa dharura wa kiutu, ambayo ni karibu nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo. Takribani nusu ya watu katika mji mkuu Bangui, ambao ni zaidi ya nusu milioni wametoroka makwao, huku wengine 100,000 wakifurika katika kambi moja ya muda katika uwanja wa ndege karibu na mji mkuu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia watoto - UNICEF lilionya mwishoni mwa mwezi Desemba, kuwa watoto wanaingizwa vitani, na likathibitisha vifo vya watoto 16 tangu Desemba 5. Wawili kati ya watoto hao walichinjwa.

Rais wa sasa Michael Djotodia ambaye alichukua mahali pa Francois Bozize baada ya mapinduzi
Rais wa sasa Michael Djotodia ambaye alichukua mahali pa Francois Bozize baada ya mapinduziPicha: STR/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Mali na Senegal zimewahamisha mamia ya raia wao wanaotoroka mapigano nchini humo. Katika mji mkuu wa Mali, Bamako, waziri anayehusika na zoezi la kuwahamisha raia, Abdramane Sylla pamoja na maafisa wengine wawili walikaribisha kundi la karibu watu 270 waliorudishwa nyumbani kwa kutumia ndege iliyokodishwa na serikali.

Waziri Sylla amesema ndege nyingine itaihamisha hii leo idadi nyingine kama hiyo ya raia wa Mali. Zaidi ya Wamali 3,000 wanalikuwa wakiishi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Lakini kufikia sasa ni 500 pekee waliosema wanataka kurudi nyumbani. Wengi wa waliohamishwa ni wanawake na watoto, wengi wao waliozaliwa nchini humo na wazazi wa Mali waliokuwa wakiishi nchini humo kwa muda mrefu.

Senegal imesema imewahamisha karibu raia 600 katika kipindi cha chini ya wiki moja, kwa mujibu wa maafisa mjini Dakar. Shirika la habari la Senegal, APS limeripoti kuwa serikali imewasafirisha raia wa Guinea, Mali na Gambia ambao walikuwa wamekwama katika mzozo wa Afrika ya Kati, lakini haikutoa idadi kamili.

Wanajeshi wakijaribu kuutuliza umati wa waandamanaji mjini Bnagui
Wanajeshi wakijaribu kuutuliza umati wa waandamanaji mjini BnaguiPicha: MIGUEL MEDINA/AFP/Getty Images

Nigeria ilisema siku ya Jumapili kuwa inawaondoa raia wake 1,600 ambao walitafuta hifadhi katika ubalozi wake mjini Bangui. Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa raslimali, imekumbwa na ongezeko la machafuko tangu mapinduzi ya mwezi Machi, ya muungano wa waasi wa SELEKA uliokuwa na waislamu wengi ulipomweka madarakani Michael Djotodia kama rais wa kwanza wa nchi hiyo Muislamu.

Ijapokuwa Djotodia alilivunja kundi hilo la waasi, baadhi yao waliendelea na vurugu, na kusababisha miezi kadhaa ya matukio ya mauaji, ubakaji na wizi, hali iliyowalazimu Wakristo kuunda makundi ya kujikinga. Majeshi ya Ufaransa na Umoja wa Afrika yamekuwa yakijaribu kurejesha utulivu katika nchi hiyo tangu yalipotwikwa mzigo huo mwezi uliopita na Umoja wa Mataifa. Zaidi ya watu 1,000 wameuawa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita pekee, wakati wengine karibu nusu milioni wakiwachwa bila makaazi, tangu mapinduzi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba