1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watakiwa kupiga vita biashara haramu ya silaha ndogo ndogo.

Mohamed Dahman1 Mei 2008

Suala la biashara haramu ya silaha ndogo ndogo yenye kusababisha maafa duniani laibuka tena Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/Dreb
Athari za biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ni kama inavyonekana hapo pichani kutumbukizwa kwa watoto vitani.Picha: AP

Umoja wa Mataifa hapo Jumatano umetakiwa kuchukuwa hatua kupambana na biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi ambazo zinahusishwa na vifo vya maelfu watu kila mwaka katika umwagaji damu unaofungamanishwa na mizozo ya ndani ya nchi na biashara ya madawa ya kulevya.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya balozi wa Slovenia kwa Umoja wa Mataifa Sanja Stiglic amesema Umoja wa Ulaya unaona kuenezwa kwa silaha za aina hiyo duniani kote ni miongoni mwa changamoto za hatari kabisa na tishio kwa utulivu na usalama duniani kadhalika kwa maendeleo na ustawi wa kiuchumi na kijamii.

Stiglic amesema Umoja wa Ulaya umejizatiti kuzuwiya kuenea na kupatikana kwa silaha hizo na risasi ambao hauna udhibiti.

Umoja wa Ulaya katika hilo umeungwa mkono na nchi kadhaa wakati wa mjadala wa ufunguzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kujadili hatua za kukomesha biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi.

Katika repoti inayotolewa mara mbili kwa mwaka kwa baraza hilo la usalama lenye nchi wanachama 15 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon amesema hakuna takwimu sahihi kabisa juu ya idadi ya silaha hizo zinazosambazwa duniani.Lakini repoti hiyo imesema duru zenye uzito zimekadiria kwamba silaha hizo zinafikia milioni 875 ikiwa ni pamoja na idadi ya silaha hizo zinazouzwa kinyume na sheria duniani kote.

Mjadala huo umelenga juu ya biashara haramu ya silaha hizo ambayo hukwepa udhibiti wa serikali wakati ikisababisha vifo duniani kote katika matumizi ya nguvu yanayotokana na mizozo ya ndani ya nchi hadi vita vidogo vidogo.Kwa mujibu wa repoti hiyo silaha hizo huwa zinaweza kuingia katika soko la magendo kwa kupitia usambazaji,wizi,kupokonya au kupotoshwa dhamira ya matumizi yake pamoja na kuuzwa upya.

Repoti inasema zaidi ya kampuni 1,000 kutoka nchi 100 zinahusika na utengenezaji wa silaha ndogo ndogo wenye thamani ya mabilioni ya dola kila mwaka.

Hatua ziliopo hivi sasa za kupiga vita biashara haramu ya silaha ni pamoja na kuziwekea alama,kuzichunguza na vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.Lakini hatua hizo hazikupunguza biashara hiyo haramu.

Hapo mwaka 2001 Umoja wa Mataifa ulipitisha mpango wa utekelezaji dhidi ya biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi lakini sio vifungu vyote vya mpango huo vimetekelezwa.

Balozi wa Afrika Kusini Dumisani Kumalo amesema silaha hizo zimekuwa silaha zinazopendelewa na wababe wa vita ambao wameweza kuwaorodhesha watoto katika mizozo ilio sugu barani Afrika.

Kumalo anasema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wajibu kuangalia upya vipi silaha ndogo ndogo zinavyochangia vibaya katika suala la kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Balozi wa Mexico katika Umoja wa Mataifa Claude Heller yeye anasema serikali yake inapendelea kuimarishwa kwa taratibu za kuziwekea alama na kuzichunguza silaha hizo kwa kuzifanya taratibu hizo kuwa lazima kutekelezwa na serikali.

Hatua hizo zinaziwezesha serikali kuzichunguza silaha hizo ili kujuwa wamiliki wake halisi.