1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wazindua hazina ya misaada, Pakistan

10 Agosti 2010

OCHA lasema mafuriko hayo ni mabaya kuliko janga la tetemeko la ardhi la Haiti mwaka huu na pigo la Tsunami la 2004.

https://p.dw.com/p/Oglx
Watu milioni 13.5 wanaathirika na mafuriko nchini Pakistan.Picha: AP

Umoja wa Mataifa umezindua hazina ya msaada kuwasaidia zaidi ya watu milioni 13 wanaoathirika na janga baya ya kibinadamu baada ya mafuriko kuyavuruga maeneo mengi Pakistan na sasa kusababisha kitisho cha mkurupuko wa magonjwa.

Ofisi inayoratibu masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa, OCHA inasema kwamba kiasi ya watu milioni 1.5 wamehamishwa kutoka kwa makaazi yao kusini mwa Pakistan na vipande vikubwa vya ardhi ya kilimo vimefunikwa na maji katikati ya mkoa wa Punjab huku eneo la kaskazini magharibi linalozongwa na mzozo wa wapiganaji wa Taliban pia likiathirika.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki Moon ametangaza kwamba umoja huo utatoa ombi la msaada wa mamilioni ya Dola ili kuushughulikia mkasa huo.

Serikali ya Pakistan na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, wametoa wito wa misaada zaidi ya uokozi na wanasema fedha nyingi zitahitajika kurejesha hali ya kawaida ya raia walioathirika na pia kujenga upya miundo mbinu.

Maeneo ya bonde la Swat, Kaskazini magharibi ambapo Pakitan ilihusika katika vita vikali dhidi ya wapiganaji wa Taliban mwaka jana, yameathirika pia na barabara zimeharibiwa.

Mratibu wa misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa, John Holmes amesema jitihada za kiutu zinafaa kuimarishwa haraka iwezekanavyo ili kuweza kukidhibiti kiwango cha janga hilo la mafuriko.

Pakistan Präsident Asif Ali Zardari vereidigt
Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan akosolewa vikali kwa kupanga ziara nje ya nchi wakati wa mkasa wa mafuriko.Picha: AP

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uratibu wa masuala ya kiutu, OCHA, Maurizio Giuliano alisema kiwango cha janga hilo ni kikubwa kwa sababu kwa kulinganisha takwimu kama nyumba zilizoharibiwa na watu walioathirika, ni ya juu kuliko athari ya tetemeko la ardhi nchini Haiti mwaka huu, pigo la Tsunami mwaka wa 2004 na tetemeko la ardhi kusini mwa bara Asia la mwaka wa 2005. Alisema watu hawawezi kutambua athari ya janga hilo kwa sababu sio watu wengi waliofariki lakini kulingana na mahitaji ya kiutu, ni janga baya zaidi.

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba watoto ndio wanaoathirika zaidi na kuna kitisho kikubwa cha mkurupuko wa magonjwa kama kipindupindu na watu 1,600 wamefariki. Umoja huo umesema kwamba mashirika ya kutoa misaada yametoa Dola milioni 38.2 na kima kingine cha Dola milioni 90.9 kimeahidiwa.

Huku hayo yakijiri, waathiriwa wamewakosoa viongozi husika kwa kushindwa kuwasaidia hivyo kuongeza mzigo kwa taifa hilo ambalo tayari linalemewa kifedha huku likijitahidi kukabiliana na wapiganaji wa Taliban. Rais Asif Ali Zardari amerejea nyumbani leo baada ya kukamilisha ziara yake wakati ambapo serikali yake inaendelea kukosolewa vikali kuhusu jinsi inavyolishughulikia janga hilo. Bw Zardari alizizuru Uingereza, Ufaransa na jana alipitia Syria. Mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji alimrushia kiatu alipokuwa nchini Uingereza.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Josephat Charo