1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa

25 Septemba 2009

Chavez ampongeza Obama .

https://p.dw.com/p/JokQ
Rais Barack Obama na Dmitry Medvedev )Picha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani, aliliacha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana,mjini New York, kuelekea Pittsburgh kwa kikao cha kundi la G-20, akiwa amepiga hatua kidogo juu ya mzozo na Iran , katika kutilia kasi kupunguzwa silaha ulimwenguni na katika mwito wake kwa Dola Kuu kuacha kugombana na badala yake, kushirikiana.

Nae waziri mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu, aliyalaumu vikali mataifa yasiojiunga na yale yalioondoka ukumbini pale Rais Mahmud Ahmadinejad wa Iran,alipokua akihutubia. Jukwaani, jana alitamba pia Rais Hugo Chavez wa Venezuela,aliempongeza rais Barack Obama, kuwa kiongozi wa matumaini kinyume na mtangulizi wake George Bush.

Mafanikio muhimu zaidi ya rais Obama, mnamo siku hizi 3 za pirika-pirika huko UM,yadhihirika ni pamoja na kuungwamkono hatimae, na rais Dimitry Medvedev wa Russia kuimarisha vikwazo dhidi ya mradi wa kinuklia wa Iran endapo ikikataa kurudi nyuma. Amefanikiwa pia kuzishawishi dola mbali mbali za kinuklia kuanza kufikiria kikweli kupunguza maboma yao ya silaha. Ingawa amepata msaada wa Russia, China bado haikuitikia kilio chake cha kukaza vikwazo dhidi ya Iran.Hatahivyo, Obama bado amejikwaa katika juhudi zake za kuutatua mgogoro wa Israel na Wapalestina.

Taarifa kutoka UM hatahivyo, zinadai lile kundi la pande 4 juu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati -(Mid-east Quartet) , lilipongeza kuwa ni hatua muhimu sana yale mazungumzo ya pande 3 alioandaa Rais Obama kati yake na waziri-mkuu Netanyahu wa Israel na Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina, Mahmud Abbas kuelekea mazungumzo mapya ya Mashariki ya Kati.

Akihutubia Baraza Kuu jana, waziri-mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel,alizilaani zile nchi ambazo, wajumbe wao hawakuungana na wenzao waliotoka nje ya ukumbi pale rais Ahmadinejad wa Iran, alipotoa hotuba yake ilioangaliwa na baadhi kuwa dhidi ya wayahudi.Netanyahu alisema na ninamnukulu,

"Kwa wale ambao walikataa kupeleka wajumbe wao ukumbini; na wale waliotoka nje ya ukumbi,pongezi kwenu.Mmetetea bayana uadilifu na mmeleta heshima kwa nchi zenu." Alisema waziri mkuu Netanyahu.Wakati wa hotuba yake juzi Jumatano, Rais Ahmadinejad wa Iran, alitaja kuwa, kuna njama kubwa na za aina mbali-mbali za mayahudi: akasema,

" Haikubaliki, kuona kikundi cha wachache kinatawala siasa,uchumi na utamaduni wa sehemu kubwa ya ulimwengu huu kupitia mtandao wake wa kutatanisha." Alidai Rais wa Iran.

Medani ilikua pia wazi jana, kwa rais Hugo Chavez wa Venezuela, aliedai kuwa mfumo wa ujamaa unaofuatwa na nchi yake Venezuela, ndio utakaotatua matatizo yote yanayolisibu bara la Amerika Kusini.Aliutaka ulimwengu kuutambua na akawataka Wamarekani kwenda kuangalia filamu iitwayo "South of the Border".

Rais Chavez,alimpongeza Rais Barack Obama akisema ameleta matumaini kwa walimwengu.

"Mungu akulinde Obama na risasi zilizomua rais John F. Kennedy"-alisema rais Chavez katika hotuba yake ndefu ambayo alihakikisha kuwa, haipindukii ile ya sahibu yake Muamar Gaddafi wa Libya.