1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UMOJA WA MATAIFA:Chad yakataa ujumbe wa UN

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLT

Serikali ya Chad inakataa kuruhusu Umoja wa Mataifa kupeleka ujumbe utakaotathmini hali nchini humo kabla kupeleka kikosi cha majeshi ya kulinda usalama.Hali hiyo inarudisha nyuma mipango ya kusaidia maelfu ya raia wa Chad wanaoathirika na mzozo unaoendelea katika eneo la Darfur nchini Sudan.

Wakati huohuo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haliwezi kuanza shughuli ya kupeleka majeshi alfu 3 ya kulinda amani kuimarisha jeshi la Umoja wa Afrika lililoko Darfur kwa sasa kwani barua kutoka kwa Rais Omar al Bashir wa Sudan inayotia nguvu hatua hiyo haijawasili.

Matatizo yanayokabili mataifa hayo mawili yalizungumziwa katika kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kilichonuia kuwaleta pamoja waasi na serikali katika meza ya mazungumzo.Kikao hicho kiliendeshwa na Jan Eliasson mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon.