1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuifunga njia ya Balkan

Admin.WagnerD7 Machi 2016

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuifunga njia ya Balkan inayotumiwa na wahamiaji kuingia Ulaya katika mkutano wa kilele unaofanyika leo (07.03.2016) mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/1I8Re
Brüssel EU Gipfel - Donald Tusk & Martin Schulz
Picha: Reuters/D. Martinez

Tangazo la kuifunga njia inayopitia mataifa ya Balkan lililoandaliwa na mabalozi wa Umoja wa Ulaya litatangazwa katika mkutano wa mjini Brussels utakaohudhuriwa pia na waziri mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

Viongozi 28 wa mataifa wanachama wataiomba serikali ya Davutoglu ikubali idadi kubwa ya wahamiaji wa kiuchumi watakaorejeshwa kutoka Ugiriki, kituo kikubwa kinachotumiwa na wakimbizi kuingilia Ulaya. Serikali ya Uturuki itatakiwa pia ifanye mengi zaidi kutekeleza makubaliano ya mwezi Novemba mwaka uliopita kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoingia katika Umoja wa Ulaya.

Davutoglu aliwaambia waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Istanbul kabla kuondoka kuelekea Brussels kwamba Uturuki imechukua hatua muhimu kutimiza majukumu yake katika mkataba wa Novemba uliokwama. Alisema idadi ya wakimbzi imepungua lakini sio kwa kasi kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendela katika taifa jirani la Syria.

Davutoglu alisema atajadiliana na viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya kuhusu juhudi za kuanza kujenga shule na hospitali kwa ajili ya wakimbizi kutumia euro bilioni tatu zilizoahidiwa na Ulaya chini ya mkataba wa Novemba.

Donald Tusk trifft Ahmet Davutoglu in Ankara
Ahmet Davutoglu, kulia, na Donald Tusk walipokutana Ankara 03.03.2016Picha: picture alliance/abaca/AA

Rais wa Jamhuri ya Czech Milos Zeman alisema Umoja wa Ulaya huapaswi kuipatia Uturuki fedha hizo kwa sababu haiko tayari na wala haiwezi kuwasaidia wahamiaji.

Davutoglu alikutana jana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na waziri mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, mjini Brussels na kuzungumzia mzozo wa wahamiaji kabla mkutano wa leo.

Ugiriki imeshuhudia Macedonia, ambayo si nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, pamoja na nchi wanachama katika njia ya upande wa magharibi mwa eneo la Balkan zikiifunga kabisa mipaka yao, hivyo kuwakwamisha wakimbizi kutoka Syria na wahamiaji wengine wanaotaka kuelekea upande wa kaskazini hadi Ujerumani na mataifa ya Scandinavia.

Ugiriki yataka wahamiaji wahamishiwe mataifa mengine

Alipowasili Brussels mapema leo, waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras, alisema, "Kwanza kabisa hili ni tatizo letu sote. Sio tatizo la nchi moja; ni tatizo la Ulaya nzima, kwa hiyo sharti tutafute suluhisho la pamoja. Ni muhimu kuharakisha mchakato wa kuwahamisha wahamiaji na tuwe na mchakato wa kuaminika."

Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya aliwaambia waandishi wa habari kwamba viongozi wa umoja huo watatangaza leo kuwa wataifunga njia ya Balkan katika siku zijazo, kukomesha mtindo wa wakimbizi kuingia kama wimbi ambao umesababisha mtafaruku na hali ya wasiwasi barani Ulaya.

Griechenland Parlament Premierminister Alexis Tsipras
Waziri Mkuu Alexis Tsipras alipolihutubia bunge la Ugiriki 24.02.2016Picha: picture-alliance/dpa/O. Panagiotou

Viongozi wa Ulaya walitarajiwa kuiunga mkono Ugiriki baada ya kuahidi wiki iliyopita kuipatia nchi hiyo euro milioni 700 kama msaada wa dharura na mataifa mengine kuisadia kuwahudumia wakimbizi wanaomiminika katika mpaka wake. Hapo jana waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alitoa wito maelfu ya wakimbizi wahamishwe haraka na kupelekwa katika mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Rais wa baraza la Ulaya, Donald Tusk, ambaye ni mwenyeji wa mkutano wa leo, alisema katika barua yake ya mualiko kwamba ufanisi utategemea kwa kiwango kikubwa mapatano na Uturuki ikubali kuwapokea wahamiaji wa kiuchumi kutoka Ugiriki ambao hawajatimiza vigezo vya kuwa wakimbizi.

Mkutano wa Brussels ulifanyika baada ya wahamiaji takriban 25, wakiwemo watoto 10, kufa maji wakati boti yao ilipopinduka walipokuwa wakijaribu kwenda Ugiriki, walinzi wa pwani ya Uturuki wamesema. Watu 15 waliokolewa nje kidogo ya mji wa bandari wa Didim nchini Uturuki jana.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre/ape

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman