1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuiregezea kamba Ugiriki ?

3 Februari 2015

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imeashiria kuwa tayari kuzifanyia marekebisho sera zake za kiuchumi lakini imegoma kufanya mabadiliko ya jumla ili kuifurahisha serikali ya nchi hiyo yenye kupinga sera ya kubana matumizi.

https://p.dw.com/p/1EV5L
Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker.
Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker.Picha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Akizungumza na bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels Jumanne (03.02.2014)Juncker amesema inabidi wazigatie kujieleza kwa njia ya kidemokrasia kulikofanywa na wananchi wa Ugiriki ambao amesema anawahusudu kwa ujasiri wao na njia wanayotumia kutenda au kutotenda kitu.

Hata hivyo amesema wale walioshinda uchaguzi nchini Ugiriki lazima watilie maanani imani na taratibu za watu wengine na kwamba sio nchi moja mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambayo imejifanyia maamuzi kwa njia ya kidemokrasia kwani pia kuna maoni mengine ya wananchi.

Amesema ndio inabidi wazifanyie marekebisho baadhi ya sera zao lakini hawatobadili kila kitu kwa sababu tu ya kuwepo kwa matokeo ya uchaguzi ambayo yamewafurahisha baadhi ya watu na kuwaudhi wengine.

Juncker ambaye zamani alikuwa waziri mkuu wa Luxembourg amesema serikali ya Ugiriki haiwezi kuutisha umoja wote wa Ulaya wenye nchi wanachama 28.

Waziri Mkuu mpya wa Ugiriki wa chama cha sera kali za mrengo wa kushoto Alexis Tsipras anatazamiwa kukutana na Mkuu huyo wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya hapo kesho kwa mazungumzo juu ya mpango wa serikali yake wa kupunguza deni lake na kumaliza sera za kubana matumizi.

Ugiriki isichonganishe nchi wanachama

Waziri wa Fedha wa Ufaransa Michel Sapin ameonya dhidi ya jaribio lolote lile la Ugiriki la kuzichonganisha Ufaransa na Ujerumani pamoja na nchi nyengine za Umoja wa Ulaya kwa kutumia mzozo huo wa madeni wa Ugiriki.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis (kushoto) na waziri mwenzake wa Ufaransa Michel Sapin mjini Paris. (01.02.2015)
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis (kushoto) na waziri mwenzake wa Ufaransa Michel Sapin mjini Paris. (01.02.2015)Picha: REUTERS/Jacques Demarthon/Pool

Amesema makubaliano kati ya Ufaransa na Ujerumani ni muhimu katika kufikia muafaka ambao utawasaidia Wagiriki na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao.

Sapin amekaririwa akisema "Sio mpango wa upande mmoja, sio Ugiriki inayojiamulia peke yake. Jambo hilo haliwezekani kwa sababu Ugiriki ni mwanachama wa kanda ya sarafu ya euro.Kwa hiyo ni suala la mazungumzo na ukweli kwamba serikali hiyo mpya ya Ugiriki inahitaji nafasi na muda kidogo hicho ni kitu cha kawaida kabisa."

Ugiriki yanadi mapendekezo yake

Serikali mpya ya Ugiriki inayoongozwa na Tsipras wa chama cha sera kali za mrengo wa kushoto cha Syriza hivi sasa inafanya ziara katika miji mkuu ya Ulaya kushawishi kuungwa mkono kwa mapendekezo yao ya kukomesha sera ya kubana matumizi.

Akizungumza na wawekezaji wa kigeni mjini London hapo jana Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis ameunadi mpango wake wa kubadilisha madeni ya Ugiriki na dhamana za serikali zenye kuchochea ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis.
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis.Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Yanis amesema "Hakuna sababu za msingi kwa nini benki ziwe na tatizo. Kitu pekee tunachohitaji kufanya kama wanasiasa barani Ulaya ni kuondowa wasi wasi wa kila mtu kwa kuonyesha nia ya pamoja ya kuweka mazingira ya utengamano katika kanda ya sarafu ya euro."

Waziri Mkuu wa Uingereza George Osborne baada ya kukutana na waziri huyo wa fedha wa Ugiriki ameuita mzozo huo kati ya Ugiriki na kanda ya sarafu ya euro kuwa ni hatari kubwa kwa uchumi wa dunia.

Mikopo ya kimataifa ya kuinusuru Ugiriki isifilisike imeiacha nchi hiyo na deni la zaidi ya euro bilioni 315 juu kwa asilimia 175 ya pato lake la jumla la ndani ya nchi.

Nchi kadhaa katika kanda ya nchi 19 inayotumia sarafu ya euro zinapinga kabisa upunguzaji wowote ule wa deni hilo la Ugiriki hususan Finland,Mataifa ya Baltik na Ujerumani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman