1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Urusi?

6 Machi 2014

NATO yaipa kisogo Urusi. Umoja wa Ulaya kuipatia Ukraine mabilioni katika mikopo. Mjini Paris, mazungumzo na Urusi yafanyika. Mgogoro wa Cremea kujadiliwa zaidi, asema waziri John Kerry

https://p.dw.com/p/1BL1H
Rais wa Urusi Vladmir Putin akiwa na rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Romopuy (kushoto), na rais wa Halmshauri ya Ulaya Manuel Barroso (kulia).
Rais wa Urusi Vladmir Putin (katikati) akiwa na rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Romopuy (kushoto), na rais wa Halmshauri ya Ulaya Manuel Barroso (kulia).Picha: Reuters

Viongozi wa serikali na mataifa ya Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo mjini Brussels Ubelgji, kuamua juu ya msaada kwa Ukraine na uwezekano wa kuiwekea vikwazo vya kwanza Urusi. Rais wa halmashauri ya Ulaya Jose Manuel Barroso alipendekeza kabla ya mkutano huo, msaada wa euro bilioni 11 kwa Ukraine, ambayo iko kwenye ukingo wa kufilisika. Misaada hiyo ya dharura hata hivyo ina masharti ambayo utawala mjini Kiev unapaswa kuyajadili na shirika la fedha la kimataifa IMF.

Msaada kupelekwa haraka
Rais huyo wa halmashauri ya Ulaya hata hivyo aliweka wazi kuwa fedha hizo zitaifikia Ukraine haraka iwezekanavyo kwa sababu inahitaji msaada wa dharura. Maafisa wa Umoja wa Ulaya tayari wapo mjini Kiev kubaini mahitaji ya kifedha na kutafakari namna ya kuzitoa fedha hizo ili zisiishie katika mikono ya wala rushwa. Umoja wa Ulaya pia unapanga kuandaa mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Ukraine. Marekani tayari imetoa dola bilioni moja katika msaada wa dharura kwa nchi hiyo. Barroso alisema matukio ya hivi karibuni yamewashtuwa wote, na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuzingatia kanuni za amani.

Bunge la Ulaya likionyesha mshikamano na Ukraine.
Bunge la Ulaya likionyesha mshikamano na Ukraine.Picha: Frederick Florin/AFP/Getty Images

"Hili linatuma ujumbe wa wazi kwa Urusi, na kusawazisha hatua zetu katika njia ambayo kwa upande mmoja tunasitisha shughuli zetu za kila siku, na kwa upande wa pili tunafungua mlango wa majadiliano ya kisiasa, tunatumaini kwamba tunaweza kuchagia katika upatikanaji wa suluhu ya kisiasa na kidiplomasia," alisema Barroso mbele ya waandishi wa habari mjini Brussels siku ya Jumatano.

Barroso alisema pia Umoja wa Ulaya unataka kuangalia uwezekano wa kuifikishia Ukraine mahitaji ya gesi kupitia mataifa ya Ulaya, ikiwa Urusi itaamua kuikatia ugavi wa nishati hiyo. Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yasenyuk atahudhuria mkutano wa leo, na kutembelea makao makuu ya jumuiya ya kujihami NATO. Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen alimuambia waziri mkuu huyo wa Ukraine baada ya mkutano wa baraza la NATO na Urusi kuwa Ukraine bado inaweza kujiunga na jumuiya hiyo.

Katika mkutano wa NATO uliofanyika mjini Bucherest mwaka 2008, jumuiya hiyo iliazimia kuzipokea nchi za Ukraine na Georgia pale zitakapokuwa tayari kujiunga nayo. Chini ya uongozi wa rais Viktor Yanukovych, Ukraine haikufuatilia mipango ya kujiunga na NATO. Rasmussen alisema ni juu ya raia wa Ukraine kuamua iwapo wanataka kujiunga na jumuiya hiyo au la. Lakini Urusi imekuwa ikikosoa vikali hatua za kuisogeza Ukraine karibu na jumuiya hiyo ya kujihami ya mataifa ya magharibi.

Mkutano kati ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na mawaziri kadhaa ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov mjini Paris jana haukuwa na mafanikio makubwa. Jitihada za mawaziri hao kuwakutanisha Lavrov na waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Andrey Deshchitsya ziligonga mwamba, kwa sababu Urusi haiitambui serikali mpya mjini Kiev.

Urusi yazidi kubinywa
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alirejelea wito wake kwa Urusi kuondoa majeshi yake katika rasi ya Cremea."Urusi ilifanya chaguo, na tumebainisha wazi kwamba ni chaguo lisilo sahihi. Ni changuo la kupeleka vikosi katika rasi ya Crimea. Urusi sasa inaweza kuchagua kuondoa majeshi yake, na sisi tuko tayari kufanya kazi na Urusi pamoja na washirika wetu, kutafuta njia ya kuyapunguza," alisema Kerry mjini Paris Ufaransa.

Wanajeshi wa Urusi walioko Cremea. Marekani na Uingereza zilishinda kuzileta pamoja Urusi na Ukraine mjini Paris siku ya Jumatano.
Wanajeshi wa Urusi walioko Cremea. Marekani na Uingereza zilishinda kuzileta pamoja Urusi na Ukraine mjini Paris siku ya Jumatano.Picha: Filipo Monteforte/AFP/Getty Images

Hadi sasa Urusi imepuuza matakwa ya Marekani, kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda G7 na Umoja wa Ulaya, ya kuondoa wanajeshi wake kutoka Crimea. Mkutano wa leo wa kilele utatathimini iwapo Urusi imechukuwa hatua zozote kupunguza mgogoro. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius alisema katika mahojiano kuwa wanapaswa kushauriana juu ya hatua ya kwanza ya vikwazo dhidi ya Urusi.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya barroso alisema hii ndiyo mara ya kwanza katika miaka mingi ambapo wanaona kitisho cha kweli dhidi ya utulivu wa bara la Ulaya, na kusema anatarajia viongozi wa Ulaya watasimama pamoja katika suala hili.

Mwandishi: Bernd Riegert
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba