1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kutayarisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi

31 Agosti 2014

Viongozi wa Umoja wa Ulaya jana Jumamosi(30.08.2014)wameamua kutayarisha haraka duru nyingine ya vikwazo dhidi ya Urusi, ikiwa ni jibu kwa ajili ya kujiingiza kijeshi kwa Urusi katika nchi jirani ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/1D4Eo
Brüssel EU Gipfel Donald Tusk und Cameron
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakati wa mkutano wao mjini BrusselsPicha: REUTERS

Wameishutumu Urusi kwa uvamizi na kuitaka nchi hiyo kuondoa mara moja majeshi yake na vifaa kutoka Ukraine.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amedai kuwa "maelfu ya wanajeshi kutoka nje na mamia ya vifaru kutoka nje " wako katika ardhi ya nchini yake.

Belgien Petro Poroschenko in Brüssel 30.08.2014
Rais Petro Poroshenko wa UkrainePicha: Reuters

"Haikubaliki kabisa kwamba wanajeshi wa Urusi wako katika ardhi ya Ukraine," waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema. "Tunafahamu kutokana na historia ya Ulaya hatari ya mipaka ya nchi ikitishiwa na kukiukwa kwa njia hii."

Vikwazo zaidi dhidi ya Urusi

"Tunapaswa kuongeza vikwazo vyetu na kusimama kwa pamoja kama Umoja wa Ulaya kwa sababu hii ndio njia pekee kuonesha kuwa tunahitaji Urusi ambayo haiingilii katika mataifa jirani kwa njia wanayofanya," waziri mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt amesema.

EU Gipfel David Cameron 27.06.2014
David Cameron wa UingerezaPicha: Reuters

''Tumefika katika sehemu hatari. Kila kitu kinaonesha kuwa sio tu Urusi kwamba inasaidia waasi wanaotaka kujitenga ," amesema rais wa Ufaransa Francois Hollande na kuongeza kuwa "Lakini vifaa muhimu na vya kisasa vimetolewa kwa waasi."

Hollande pia amesema washauri wa Urusi wanawasaidia wanaotaka kujitenga nchini Ukraine, lakini ameongeza kuwa ushahidi wa hatua za Urusi bado haujawekwa pamoja.

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema inaamini , "zaidi ya " wanajeshi 1,000 wa Urusi wanapigana pamoja na wanaotaka kujitenga. Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amepuuzia picha za satalaiti za NATO kuwa zina vigezo vile vile vya michezo ya kompyuta.

Francois Hollande
Rais Francois Hollande wa UfaransaPicha: Reuters

Viongozi wa Ulaya wasimama pamoja

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kutayarisha duru mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi katika muda wa wiki moja ijayo.

Wameomba hususan orodha ya "kila mtu na taasisi inayohusika na makundi ya wanaotaka kujitenga katika jimbo la Donbass," jina la kihistoria la majimbo yanayokabiliwa na mapigano ya Donetsk na Luhansk.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema vikwazo vipya vinapaswa kulenga sekta za ulinzi, huduma za kifedha na sekta ya nishati.

Hollande na viongozi wengine wamesisitiza kwamba wanajaribu kuishawishi Urusi kutafuta suluhisho la kisiasa katika mzozo huo.

Kansela wa Austria Werner Faymann amedai hapo mapema kuwa vikwazo sio , "silaha mjarabu," akidokeza kuwa vikwazo ambavyo tayari vinatekelezwa na Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi, vimeshindwa kuleta matunda yaliyotarajiwa.

Lawrow kündigt einen neuen Hilfskonvoi für die Ukraine an Archivbild 03.05.2014
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei LavrovPicha: Jure Makovec/AFP/Getty Images

"Inaonekana kana kwamba rais Vladimir Putin, kwa kiasi hadi sasa, hajaathirika na vikwazo ambavyo vimewekwa na Umoja wa Ulaya ama mataifa mengine," amesema waziri mkuu wa Ireland Enda Kenny.

Wakati huo huo Marekani imeeleza kuunga kwake mkono jana Jumamosi (30.08.2014)tangazo la viongozi wa Umoja wa Ulaya kuipa Urusi wiki moja kubadilisha mkondo wa mambo nchini Ukraine ama itakabiliwa na duru mpya ya vikwazo.

"Tunakaribisha msimamo wa pamoja wa baraza la Umoja wa Ulaya leo kuonesha uungaji wake mkono mkubwa kwa Ukraine, na mipaka ya nchi hiyo na kutayarisha vikwazo zaidi kwa ajili ya kutafakari kuchukua hatua zaidi katika siku zijazo," amesema msemaji wa usalama wa taifa nchini Marekani Caitlin Hayden.

Ameongeza kuwa , "tunafanya kazi kwa karibu na Umoja wa Ulaya na washirika wengine kuiwajibisha Urusi kwa hatua zake kinyume na sheria nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo zaidi."

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Daniel Gakuba