1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sweden na Slovenia zaimarisha mipaka yake

Admin.WagnerD12 Novemba 2015

Viongozi wa mataifa ya umoja wa Ulaya leo wanatarajia kufikia makubaliano juu ya kushirikiana kwa pamoja na mataifa ya Afrika katika jitihada za kushughulikia kukabiliana na wimbi la wakimbizi .

https://p.dw.com/p/1H4SF
Viongozi wa Umoja wa ulaya na Afrika wanaokutana nchini Malta
Viongozi wa Umoja wa ulaya na Afrika wanaokutana nchini MaltaPicha: picture-alliance/dpa/A. Babani

Hatua hii inakuja mnamo wakati mataifa ya Sweden na Slovenia yakichukua hatua katika siku za hivi karibuni za kuimarisha mipaka yao ili kukabiliana na wimbi hilo la wakimbizi ambalo linaonekana kuwa kubwa tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia.

Viongozi hao wanaokutana katika mkutano wa kilele huko mjini Valleta nchini Malta hii leo wanatarajia kusaini makubaliano ya mpango mkakati wa kukabiliana na suala hilo la wakimbizi utakaoendana na kutengwa kwa fungu la fedha kutoka katika umoja huo wa ulaya kwa ajili ya kushughulikia matatizo yanayosababishwa na kuwepo kwa wakimbizi ambayo ni pamoja na umasikini na migogoro ya kivita.

Mkakati huo pia uataenda sambamba na kuwarejesha wanakotoka baadhi ya wakimbizi wasiokuwa na hadhi ya kupewa hifadhi ya kisiasa pamoja na kuwadhibiti wafanyabiashara ya usafirishaji wahamiaji kwa njia zisizo halali.

Fungu la fedha kutengwa kushughulikia suala hilo

Katika kufanikisha mpango huo halimashauri ya Umoja wa Ulaya inatarajia kutenga fungu la fedha zenye thamani ya sarafu ya euro kiasi cha bilioni 1.8 sawa na dola za Marekani bilioni 1.9 na hivi sasa inajaribu kuyashawishi matataifa wanachama wa umoja huo kuidhinisha fedha hizo ingawa vyanzo barani humo vinaonyesha kutokuwepo kwa uhakika wa kukubaliwa kwa ombi hilo.

Naye Rais wa halimashauri ya ulaya Jean- Claude Junker alisisitiza juu ya umuhimu wa mataifa wanachama wa umoja huo kuunga mkono mpango huo.

Kwa upande wake Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara alisema ya kuwa hali ya sasa inatokana na kutokuwepo mazingira rafiki kuhusiana na taratibu za uhamiaji na hivyo kuwepo haja ya kuwepo taratibu za kisheria zikazo rahisisha upatikanaji wa hadhi ya uhamiaji na pia watu kuweza kuingia na kutoka kati ya mabara hayo pasipo vizuizi visivyokuwa na msingi.

Aidha Rais wa kamisheni ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma tatizo lilipo sasa linasababishwa na baadhi ya mataifa barani Ulaya kutokuchukua hatua mathubuti za kusaidia kupunguza tatizo hili.

Masuala mengine yanayohusiana na mipango mingine ya kukabiliana na wimbi hilo la wakimbizi yatakayo ihusisha Uturuki pia yatajadiliwa wakati viongozi hao wa umoja wa ulaya watakapokutana baadaye hii leo pasipo kuwashirikisha viongozi wa mataifa ya Afrika.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman