1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na Marekani wawashinikiza Abbas na Netanyahu kuzungumza

1 Oktoba 2010

Marekani na Jumuiya ya Ulaya wanakimbilia kuyanusuru mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yayonakaribia kukata roho, kutokana na uamuzi wa Israel kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi

https://p.dw.com/p/PSLI
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine AshtonPicha: AP

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton, na mjumbe maalum wa Marekani katika mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Seneta George Mitchell, wamekuwa kama wakimbiaji kwenye mbio za foliti. Kila mmoja anakimbia kwa kasi, ili afikie shobe kabla hajachelewa.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton (kushoto) na Waziri Mkuu wa Palestina, Salam Fayyad
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton (kushoto) na Waziri Mkuu wa Palestina, Salam FayyadPicha: AP

Asubuhi ya leo, Bi Ashton alikutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Jerusalem. Hapo ilikuwa ni muda mchache tu baada ya Netanyahu kukutana na Seneta Mitchell. Naye Seneta Mitchell alipomaliza mazungumzo na Netanyahu tu, akakimbilia Ramallah kuzungumza na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas. Bi Ashton alikuwa kwa Abbas jana na leo kabla hajaondoka Ramallah alizungumza pia na Waziri Mkuu wa Palestina, Salam Fayyad.

Wawili hawa hawataki kupitwa na hata dakika moja. Wanachokitafuta ni uthibitisho kwamba mazungumzo yataendelea. Lakini mazungumzo yenyewe, kwa hakika, yanaonekana yapo kwenye kitanda cha mauti kwa sababu ya hatua ya Israel kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Mashariki ya Kati, George Mitchell, (kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Mashariki ya Kati, George Mitchell, (kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Lakini mwenyewe Netanyahu hataki kuona kuwa ujenzi ndio uwe kikwazo. Anasisitiza dhamira ya kuendelea na mazungumzo na Rais Abbas, kwani hatimaye wote wanaongozwa na nia ya kuleta amani ya kudumu baina yao. Kauli kama hiyo pia inatolewa na Seneta Mitchell, anayesema kwamba, wanachokifanya sasa ni kutafuta mambo yanayoziunganisha pande hizi mbili ili mazungumzo yasonge mbele.

Kwa upande mmoja, Seneta Mitchell na Bi Ashton wanamshawishi Rais Abbas abakie kwenye mazungumzo licha ya kuendeleza ujenzi wa makaazi ya walowezi. Kwa upande mwengine, wanamshawishi Netanyahu afute amri ya uendelezaji wa ujenzi huo. Lakini hadi sasa, Netanyahu ameshikilia msimamo wake wa kutokuzuia ujenzi na Rais Abbas hajatoa kauli rasmi ya ama kubakia au kujiondoa kwenye mazungumzo.

Kwa hivyo, hiki ni kipindi cha majaribu kwa pande zote zinazohusika. Kwa Abbas, ni kipimo cha uongozi wake: akiridhia kubakia kwenye mazungumzo, ataonekana msaliti na jamii kubwa ya wananchi wa nchi za Kiarabu na za Kiislam, lakini akikataa, atapoteza imani ya serikali za mataifa ya Magharibi na zile za marafiki zao katika nchi za Kiarabu. Kwa Netanyahu, akikubali kuzuia ujenzi, atakuwa anauweka rehani mustakabali wake wa kisiasa nchini mwake, akikataa anapoteza fursa ya amani na Wapalestina, ambayo huenda ikaletwa na mafanikio ya mazungumzo haya.

Kwa Marekani, kupatikana kwa amani katika eneo hili ni turufu kubwa kwa Rais Barack Obama, ambaye amefika umbali wa kutoa ahadi ya ulinzi kwa Israel pindi ikikubaliana na usitishaji wa ujenzi, na yakishindwa ni ushindi kwa wapinzani wa siasa za Obama kuelekea Mashariki ya Kati. Kwa Umoja wa Ulaya, mgogoro wa Mashariki ya Kati lazima umalizike haraka, maana wachunguzi wanaona kuwa pana uhusiano baina ya migogoro kama hii katika nchi za Kiarabu na za Kiislam na vitisho vya mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Ulaya.

Mchezo huu wa tega nikutege, haujulikani mwishowe utakuwa na jawabu gani!

Mwandishi: Mohammed Khelef/Hazel Ward/AFP

Mhariri: Josephat Charo