1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na tuzo ya amani ya Nobel

Admin.WagnerD10 Desemba 2012

Kamati ya tuzo ya amani ya Nobel leo itaukabidhi Umoja wa Ulaya tuzo ya Nobel kwa mwaka 2012. Lakini je, umoja huo ulistahili kupewa tuzo hiyo kweli?

https://p.dw.com/p/16z25
Umoja wa Ulaya
Umoja wa UlayaPicha: Reuters

Mwenyekiti wa Kamati ya Nobeli, Thorbjörn Jagland alipotangaza uamuzi wa kamati hiyo Oktoba 12 mjini Oslo, hadhira iliitikia kwa minong'ono ya kushangazwa. Lakini Kamati hiyo ilisema uamuzi wake ulikuwa na maana. Umoja wa Ulaya ulistahili tuzo hiyo kwa sababu umoja huo na watangulizi wake wamechangia kwa zaidi ya miongo sita, katika kuendeleza amani, maridhiano, demokrasia na haki za binaadamu barani Ulaya.  Na kwa mujibu wa kamati hiyo, hayo ndiyo yaliyokuwa matokeo muhimu ya Umoja huo. Na leo hii, Umoja wa Ulaya unakabidhiwa tuzo yake mjini Oslo, Norway.

Mwenyeketi ya kamati ya Nobel Thötbjern Jagland wakati akitangaza mshindi wa tuzo ya Nobel ya mwaka huu wa 2012.
Mwenyeketi ya kamati ya Nobel Thötbjern Jagland wakati akitangaza mshindi wa tuzo ya Nobel ya mwaka huu wa 2012.Picha: picture-alliance/dpa

Bila shaka haya ni mambo ambayo raia wengi wa Ulaya wanachukulia kimzaha, katika wakati ambapo shughuli za kila siku za taasisi nyingi za Umoja wa Ulaya zinahusisha kupambana na mambo magumu yanayohusu soko la pamoja, kulinda walaji, au kunusuru sarafu ya euro. Lakini kwa mujibu wa kamati ya Nobeli, hata kama ulikuwa mchakato wa maridhiriano kati ya Ufaransa na Ujerumani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, kuingizwa kwa mataifa ya zamani ya kiosovieti baada ya kuvunjwa kwa ukuta wa Berlin, au ndoto ya Ulaya kwa mataifa mengi ya Balkan ya magharibi, kazi ya utulizaji iliyofanya na Umoja wa Ulaya imesaidia kubadilisha sehemu kubwa ya Ulaya kutoka bara la vita na kuwa bara la amani.

Uamuzi ulikuwa kama onyo

Wawakilishi rasmi wa Umoja wa Ulaya walifurahishwa na tuzo hiyo na hawakuwa na tatizo la kuelewa maelezo. Rais wa Umoja wa Ulaya Herman van Rompuy alikwenda mbali zaidi kwa kuuita Umoja wa Ulaya taasisi kubwa zaidi ya amani kuwahi kuwepo katika historia ya ulimwengu. Rais wa Halmashauri ya umoja huo, Jose Manuel Barroso, alijiwakilisha kama rafiki wa watu wa kawaida na kusisitiza kuwa tuzo haikutolewa kwa taasisi za umoja huo na mataifa wanachama wake, bali pia kwa raia wote milioni 500 wa Umoja wa Ulaya. Ni Barroso iliyetaka kutumia tuzo hiyo ya Nobel kumaliza hali mbaya ya mgogoro wa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya. "Tuzo ya Nobel inaonyesha kuwa hata katika wakati mgumu, Umoja wa Ulaya unabaki kuwa mhasishaji kwa mataifa na watu duniani kote, na kwamba jumuiya ya Kimataifa inahitaji umoja wa Ulaya ulio imara," alisema Barroso.

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy
Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van RompuyPicha: Reuters

Lakini siku chache baadaye, akizungumza katika mahojiano na gazeti la Tagesspiegel am Sonntag la mjini Berlin, Jagland alionya juu ya kuanguka kwa Umoja wa Ulaya, na kusema kuwa kamati ya Nobel ilitumia uamuzi wake kuonyesha hatari iliyopo, kwamba kama Umoja wa ulaya utafeli, soko la pamoja litasambaratika. Hakuna anayejua nini kitakachotokea baada ya hapo.

Nini kilitokea kwa uhamasishaji?

Wakosoaji wa tuzo hiyo wanasema Umoja wa Ulaya hautekelezi matarajio ya tuzo hiyo. Miongoni mwa sababu wanazotoa ni pamoja na kushindwa kuwasaidia wakimbizi na uuzaji mkubwa wa silaha kwa maeneo yenye migogoro. Wanaongeza kuwa Umoja wa Ulaya haukufanya vya kutosha kuzuia mgawanyiko wa kijamii kuongezeka barani Ulaya. Wengine wanadhihaki uamuzi wa kamati ya Nobel, kama Nigel Farage kutoka Uingereza ambaye aliita tuzo hiyo kuwa ni utani wa siku ya wajinga duniani.

Lakini huo ni mfano uliopitiliza, na idadi ya watu wanaofikiri kama mbunge wa bunge la Ulaya, Rebecca Harms kutoka chama cha Kijani cha Ujeumani inachukuliwa kuwa kubwa. Siku chache baada ya kutolewa kwa tangazo, na baada ya mkutano wa Umoja wa Ulaya, aliulizwa kuhusiana na hali katika mkutano huo na yeye aliuliza katika hali ya kutoamini, kwamba nini kilitokea?

Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: dapd

Baadhi hawatahudhuria kwa maksudi

Suala la nani angekwenda kupokea tuzo hiyo leo mjini Oslo nalo lilisababisha mzozo. Rais wa Baraza la Ulaya, Herman van Rompuy, rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso na rais wa bunge la umoja huo, Martin Schulz, walikubaliana kwa haraka kwamba wote watakwenda kwa pamoja. Lakini nani atakuwa wa kwanza kumshika mfalme mkono? Na nani atatoa hotuba? Na kama wote watafanya hayo, ni katika mpangilio upi?

Suala lingine lilikuwa ni wepi watakaohudhuria miongoni mwa wakuu 27 wa nchi na serikali? Kansel Angela Merkel wa Ujerumani alisema wote 27 wanapaswa kuwepo. Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema angeenda tu kama wengine wote watakuwepo. Lakini sasa amekubali kwenda hata kama kutakuwepo theluthi mbili tu ya viongozi wa Umoja wa Ulaya. Hakuna aliyeshangazwa kusikia kuwa mkosoaji wa umoja huo, waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, hatahudhuria sherehe hiyo. Mwenzake wa  Jamhuri ya Cheki, Vaclas Klaus, naye hatohudhuria. Je, kweli Umoja wa Ulaya ni mradi wa tuzo ya amani kwa ulimwengu?

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron.Picha: Reuters

Mwandishi: Hasselbach Christoph/ Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo